Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dhahabu za Sh345.9 bilioni zawaponza wafanyabiashara, wasomewa mashtaka 42

Picha Dhahabu Data Dhahabu za Sh345.9 bilioni zawaponza wafanyabiashara, wasomewa mashtaka 42

Tue, 20 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wafanyabiashara saba wa madini ya dhahabu wameburutwa mbele ya Mahakama ya Hakimu mkazi Geita na kusomewa mashtaka 42 za makosa mbalimbali ikiwemo kuunda na kuongoza genge la uhalifu, uhujumu na kutakatisha fedha.

Waliofikishwa mahakamani leo Juni 19, 2023 ni Makalanga Bukene (25) ambaye ni mshtakiwa wa kwanza ambaye anakabiliwa na mashtaka 37 kati ya mashtaka 42 yaliyosomwa mahakamani.

Washtakiwa wengine ni Sindano Robert, Bahame Kisinza, Hassan Juma, Sungwa Mbusi, Sondi Misuzi na Yusufu Mamboleo ambao wanakabiliwa na mashataka tofauti kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa mbele ya Hakimu Mkazi Geita, Johari Kijuwile.

Akisoma hati hiyo ya mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Yamiko Mlekano akisaidiana na mwenzake Scolastica Teffe amedai makosa hayo yalitendeka katika maeneo tofauti ya mikoa Shinyanga, Mbeya, Geita, Mwanza na Dar es salam.

Miongoni mwa makosa yanayowakabili washtakiwa ni kuunda genge la uhalifu na kufanya vitendo vya kihalifu ikiwemo biashara haramu ya madini kinyume na kifungu cha 18(1)4a ya Sheria ya Madini na aya ya 27 jedwali la 1 kifungu cha 57(1&2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi.

Wakili Mlekano amedai makosa hayo yalifanyika katika siku tofauti kati ya Februari Mosi, 2018 na Juni Mosi, 2023.

Mshtakiwa wa kwanza katika shauri hilo, Makalanga Bukene (25) anayetetewa na Wakili Sylvanus Joseph anadaiwa kushikirikiana na wenzake kuhujumu uchumi kwa kufanya biashara ya kuuza kilo 2, 348 za madini ya dhahabu zenye thamani ya Sh345.9 bilioni bila kuwa na leseni.

Makosa hayo yanadaiwa kutendeka kwa siku na maeneo tofauti ya mikoa ya Mbeya, Geita, Mwanza na Shinyanga.

Washtakiwa hao pia wanadaiwa kuisababishia hasara ya zaidi ya Sh24.2 bilioni Tume ya Madini kwa kukosa mapato kupitia mrabaha na tozo ya ukaguzi wa madini.

Katika kipindi hicho, washtakiwa pia wanadaiwa kuisababishia Tume ya Madini hasara ya Sh1.3 bilioni kupitia ushuru wa huduma, Service lavy.

Katika shtaka lingine, mshtakiwa wa kwanza anadaiwa kununua viwanja katika maeneo tofauti mkoani Geita na Mwanza akitumia fedha haramu zilizotokana na vitendo vya kufanya biashara bila leseni na kukwepa kodi.

Mshtakiwa wa kwanza pia anadaiwa kushirikiana na wenzake ambao hawakuwepo mahakamani kugushi nyaraka za uongo na kuziwasilisha ofisi ya Msajili wa Hati Mkoa wa Geita kwa lengo la kubadilisha umiliki wa ardhi. Makosa hayo yanadaiwa kutendeka Septemba 23, 2022.

Desemba 30, 2022 mshatakiwa wa nne katika shauri hilo anadaiwa kuhamisha kutoka benki Sh50 milioni kwenda akaonti ya mtu anayefahamika kwa jina la Doto Bukene huku ukifahamu kuwa fedha hizo ni zao la uhalifu.

Mshtakiwa wa tano, Sungwa Mbusi amedaiwa kuwa akiwa eneo la Soko la Dhahabu Wilaya ya Chunya, alikutwa na Sh91 milioni zilizotokana na kuundwa kwa kwa genge la uhalifu.

Shtaka lingine linalomhusu Sondi Misuzi ni kukutwa Sh12 milioni akiwa eneo la soko dogo la madini Wilaya ya Chunya; fedha zinazodaiwa kupatikana kupitia vitendo vya kihalifu.

Katika shtaka lingine, washtakiwa wakiwa maeneo tofauti ya mkoa wa Mbeya, Geita, Kahama, Mwanza na Dar es Salaam waliuza dhahabu yenye thamani ya Sh2.8 bilioni bila kuweka rekodi huku wakijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kisheria kusikiliza shauri hilo na wamerejeshwa mahabusu hadi Julai 3, 2023 shauri hilo litakapotajwa tena.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live