Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dereva wa halmashauri anayedaiwa kusafirisha ‘unga’ kwa gari la Serikali yamkuta

Ab34385a953794473f1afecc5fd9b47c Mfano wa dawa za kulevya

Thu, 12 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Halmashauri ya Jiji la Arusha imemsimamisha kazi dereva Athuman Magio, kwa tuhuma za kutumia gari la halmashauri hiyo kusafirishia dawa za kulevya.

Akizungumza juzi kwenye kikao cha Baraza la Madiwani Mkurugenzi wa jiji hilo, Dk John Pima, alisema amechukua hatua hiyo baada ya baraza la madiwani kujigeuza na kuwa kamati maalumu ya kujadili nidhamu ya mtumishi huyo.

Pima alisema tukio hilo ni la Mei 2, mwaka huu na alikamatwa wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro akituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya.

Alisema siku ya tukio, dereva huyo akiendesha gari Toyota Land Cruiser yenye namba za usajili STJ 7333 asubuhi alitumwa kwenda wilayani Karatu kuwachukua maofisa wa halmashauri hiyo waliokuwa kwenye shughuli za kikazi.

Kwa mujibu wa mkurugenzi, dereva huyo aliporudi Arusha, aliegesha gari kwenye ofisi za jiji na kulikabidhi kwa walinzi kwa kuliandikisha kwenye kitabu cha walinzi.

Alisema ilipofika jioni, alirudi kuchukua gari hilo na kuwadanganya walinzi kwamba alikuwa akiendelea na kazi, hivyo walimruhusu na kuondoka hadi wilayani Rombo alikokamatwa na polisi waliokuwa doria.

Mkurugenzi alisema mtumishi huyo alisimamishwa kazi na yupo mikononi mwa polisi mkoani Kilimanjaro. Alisema kitendo alichofanya, ni kinyume na kanuni za utumishi wa umma.

Katika hatua nyingine, halmashauri ya Jiji la Arusha imekusanya asilimia 80 ya bajeti yake ambayo ni Sh bilioni 23.

Pia baraza limeagiza halmashauri kuongeza udhibiti wa mapato kwa kuziba mianya iliyopo.

Mkurugenzi alisema halmashauri hiyo katika kipindi hicho, imejenga shule, zahanati vituo vya afya na jengo la utawala huku upatikanaji wa dawa za binadamu ukiwa ni asilimia 96 kwenye vituo vya afya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live