Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dereva ‘mtoto, mzee’ akikutwa na school bus faini Sh250,000

20600 PIC+DEREVA TanzaniaWeb

Thu, 4 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bagamoyo.  Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limesema litamtia hatiani dereva yeyote mwenye umri chini ya miaka 35 na anayezidi miaka 60, atakayekutwa akiendesha basi linalobeba wanafunzi maarufu kama ‘school bus’.

Akizungumza wakati akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari leo Septemba 3, Mwanasheria wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Deus Sokoni amesema utaratibu huo umewekwa kwa mujibu wa sheria ya leseni ya usafirishaji sura ya 317 katika tangazo la Serikali namba 421 kanuni namba 27 (1) (C).

Amesema suala hilo pia limetafsiriwa katika sheria ya 27 kwamba basi hilo lazima liwe zima, liwe na leseni ya kufanya shughuli hiyo na lenye rangi ya manjano.

 

“Mamlaka ya Udhibiti na Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) ina wajibu wa kutoza Sh250,000 kwa dereva yeyote mwenye umri chini ya miaka 35 atakayekutwa anaendesha basi la wanafunzi, umri sahihi uliowekwa ni miaka 35 mpaka 60,” amesema Sokoni.

Sokoni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bloomberg inayosimamia kampeni ya usalama barabarani nchini kwa ushirikiano na Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani (WHO) amesema trafiki wanapaswa kuyakagua magari hayo na wakimkamata dereva inapaswa kulipishwa faini ya Sh30,000 na sheria ya Sumatra inataja kiasi cha Sh250,000.

Amesema wamewapa oda wamiliki wote wa shule mambo ya kuzingatia iwapo magari ya kubeba wanafunzi yanatumika katika shule zao.

“Katika moja ya sheria na kanuni lazima dereva ajue maeneo yote anayopita kuacha watoto, barabara ikoje, dereva wa Lucky Vincent hakujua barabara anayoendesha ikoje, hakujua kama kuna hatari mbele hivyo ajali ilitokea,” amesema.

Amesema licha ya kikosi cha usalama kutoa mafunzo kwa shule kadhaa jijini Arusha, Dar es Salaam na mikoa mingine, bado shule nyingi Tanzania wanawapa jukumu la kuendesha magari ya wanafunzi watu wasiokuwa na elimu ya udereva na umri unaotakiwa.

“Tumekuwa tukitoa elimu hii na ni ya mwendelezo na maelekezo ya serikali ukiwa na shule unatakiwa kujisajili Sumatra na lazima iwe imekaguliwa na kila shule zikifungwa lazima zikaguliwe, asiyefanya hivyo sisi tunamfuata moja kwa moja kwani anakuwa amekiuka maelekezo.”

Akitoa mafunzo, mwandishi maarufu kutoka nchini Marekani, Tom Hundrey amewataka waandishi nchini Tanzania kuangalia namna ya kuandika habari zenye masuluhisho kuhusu masuala ya usalama barabarani huku kipaumbele kikiwa namna ya kuangalia usalama kwa watoto.

“Kuandika habari za usalama barabarani zenye masuluhisho ni namna nzuri ya kupunguza ajali zinazoweza kuzuilika, lakini pia mtaisaidia Serikali kuona namna sahihi ya kuweka miundombinu na kurekebisha sheria zilizopo,” amesema Hundrey.

Chanzo: mwananchi.co.tz