Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, linamshikilia dereva Bajaji Abdan Abdi, mkazi wa Majengo kwa Mtei, Manispaa ya Moshi, kwa tuhuma za mauaji ya Michael Dastani Ngulizi, aliyekuwa mlinzi ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi.
Mlinzi huyo mwenye umri wa miaka 55, alikuwa ni askari wa Jeshi la akiba (Mgambo), na alifariki dunia Julai 21 mwaka huu, baada kudaiwa kujeruhiwa na Abdi (21) na hivyo kusababisha kifo chake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo baada ya mtuhumiwa huyo kukataa kukamatwa kwa kosa la kufanya fujo na kuwatishia ndugu zake.
"Tukio hili limetokea Julai 21, 2023 majira ya saa 6:30 mchana huko maeneo ya Majengo kwa Mchomba, Kata ya Majengo, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, ambapo marehemu alijeruhiwa na kitu chenye ncha kali ubavuni," amesema na kuongeza;
"Kufuatia tukio hili, tunamshikilia Abdan Mohamed Abdi, (24), dereva bajaji kwa tuhuma za kusababisha kifo cha Michael Dastani Ngulizi, (55), askari wa Jeshi la Akiba (Mgambo) ambaye pia ni mlinzi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi."