Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dereva anayedaiwa kuwatelekeza wahamiaji haramu Morogoro mbaroni

43947 Pic+dereva Dereva anayedaiwa kuwatelekeza wahamiaji haramu Morogoro mbaroni

Tue, 26 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Mtu mmoja Raia wa Kenya, Johnson Kimath (37) anayedaiwa kuwa dereva na mkazi wa Machakosi, anashikiliwa na Polisi Mkoani Morogoro kwa tuhuma za kuwasafirisha wahamiaji haramu na baadaye kuwatelekeza.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa Februari 20, 2019 akiwa katika harakati za kuvuka mpaka wa Tunduma nchini Tanzania akielekea Zambia.

Mwishoni mwa mwaka jana, Waethiopia 23 waliokuwa wakisafirishwa kwenda nchini Afrika ya Kusini walikutwa wametelekezwa na 14 wakiwa wamefariki katika kijiji cha Sangasanga wilayani Mvomero.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa amewaambia waandishi wa habari leo Februari 26, 2019 kuwa mtuhumiwa amekamatwa na Polisi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama na alikuwa akiendesha gari lenye namba ya za usajili  CK12458 iliyotolewa Septemba 5, 2018 nchini Kenya.

“Amekamatwa mpakani wakati akikaguliwa hati yake ya kusafiria (Passport) ndipo ilipoonyesha alikuwa akitafutwa na vyombo dola kwa kosa la kusafirisha wahamiaji haramu,” amesema kamanda huyo.

Amesema Desemba 12,2018 saa saba mchana huko eneo la kwa Mwarabu Kijiji cha Sangasanga barabara ya Iringa-Morogoro Waethiopia hao walitelekezwa na derena huyo.

Amesema baada ya tukio hilo, msako mkali ulifanyika kwa kushirikiana na wananchi na ilipofika Desemba 31, 2018 walifanikiwa kukamata gari lenye namba za usajili VZW 720GP aina ya Nissan Diesel UD90, ikiwa imetelekezwa jirani na nyumba ya kulala wageni iliyopo eneo la Melela Mlandizi na dereva hakuwapo.

Kamanda Mutafungwa amesema dereva huyo anaendelea kuhojiwa na hatua za kufikishwa mahakamani zitafuata.

Wakati huo huo, Kamanda Mutafungwa amesema Waethiopia 14 waliofariki dunia na maiti zao kuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, maiti tano tayari zimeshachukuliwa na ndugu huku 9 zikiwa bado zimehifadhiwa zinasubiri ndugu.

Jeshi la polisi limetoa wito kwa  wananchi kuacha kujihusisha na biashara ya usafirishaji wahamiaji haramu na wale watakaojihusisha na biashara hiyo watakamatwa na kufikishwa mahakamani.

 

Mwisho.



Chanzo: mwananchi.co.tz