Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dawa za kulevya zawatupa jela maisha raia wawili wa Latvian

Hukumu Pc Data Dawa za kulevya zawatupa jela maisha raia wawili wa Latvian

Tue, 13 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Raia wawili wa Latvian, Linda Mazure na Martins Pravins, wamehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam.

Wakati mshtakiwa wa kwanza, Linda Mazure alikamatiwa JNIA wakati mizigo yake ilipokaguliwa katika mashine ya ukaguzi, mshirika wake, Martins aliyekuwa mshtakiwa wa pili alikamatwa katika hoteli ya Irsis iliyoko Kariakoo, jijini Dar es Salaam walipokuwa wamefikia.

Linda alikamatwa JNIA Aprili 17, 2019 baada ya mabegi yake mawili aliyokuwa akisafiri nayo, kupitishwa katika mashine na kugundulika kuwa na kilo 4.87 za dawa aina ya heroine, alizokuwa azisafirishe kwenda Warsaw, nchini Poland kupitia Doha.

Hukumu hiyo ambayo nakala yake imepatikana leo Februari 13, 2024 katika mtandao wa Mahakama, ilitolewa Ijumaa iliyopita na Jaji Ephery Kisanya wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi jijini Dar es salaam.

Kuthibitisha shtaka dhidi yao, upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa Serikali, Moses Mafuru akisaidiana na mawakili wa Serikali Elizabeth Mwanga, Blandina Mnung’a na Nitike Mwaisaka, uliita mashahidi sita na kuwasilisha vielelezo 17 vya kesi hiyo.

Walivyokamatwa

Ushahidi uliotolewa mahakamani, ulieleza Aprili 17,2019, ofisa usalama, Joseph Nyambale, akiwa katika mashine ya ukaguzi, aliona mabegi mawili yamepita kwenye mashine zikiwa na vitu ambavyo vilikuwa haviruhusiwi kusafirishwa.

Kwa idhini ya mshtakiwa wa kwanza, Linda, maofisa usalama walikata begi hilo na kulifungua ambapo ilibainika uwepo wa paketi zilizotiliwa shaka, ambapo baada ya Linda kuthibitisha ni mabegi yake, alipelekwa kituo kidogo cha Polisi JNIA Terminal II.

Katika mahojiano, mshtakiwa aliwaeleza polisi kuwa yeye ni raia wa Latvian na alifika nchini akiwa na mtu mwingine ambaye yuko hoteli ya Iris, Kariakoo ambapo polisi walikwenda katika hoteli hiyo na kumkamata mshtakiwa wa pili, Martins Pravins.

Baadaye uchunguzi wa kimaabara ulibaini mabegi yale yalikuwa na dawa za kulevya.

Katika utetezi wake mahakamani, Linda alijitetea kuwa alikuja nchini kama mtalii na kwamba walikutana na mshtakiwa wa pili kwenye ndege wakija nchini na wote wawili walifikia hoteli ya Iris, na alishindwa kwenda Hifadhi ya Serengeti baada ya kuishiwa.

Linda alijitetea kuwa Aprili 17, 2019 alipanga kurejea Latvia kupitia JNIA na kwamba ingawa alikiri kukabidhi mabegi yake kwa ajili ya ukaguzi, alikana kuwa na dawa za kulevya na kueleza kuwa ni muongoza mashine ndiye alimweleza juu ya jambo hilo.

Kwa upande wa mshtakiwa wa pili, yeye alijitetea kuwa aliwasili nchini Aprili 11, 2019 kwa ajili ya shughuli za utalii na kwamba alisafiri peke yake na alikutana na mshtakiwa wa kwanza baada ya kutua Doha, kabla ya kupanda ndege kuja Dar es Salaam.

Baada ya kufika Dar es Salaam, walifikia hoteli ya Iris na kukaa vyumba tofauti na kwamba Aprili 17,2019 alipanga kwenda safari kutalii Aprili 20, lakini hata hivyo siku moja kabla ya safari yake hiyo alikamatwa na kushtakiwa kusafirisha dawa za kulevya.

Hukumu ya Jaji ilivyokuwa

Katika hukumu yake, Jaji Kisanya alisema ushahidi wa kimaabara wa sampuli zilizochukuliwa katika mabegi ulithibitisha dawa zile zilizokutwa katika mabegi ya Linda pale JNIA yalikuwa na kilo 4.87 za dawa aina ya heroin hydrochloride.

Alisema swali ambalo linatakiwa kujibiwa na mahakama ni kama washtakiwa walikuwa wakisafirisha dawa za kulevya, na kusema ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri umethibitisha dawa hizo zilikutwa katika mabegi ya Linda akisafiri kwenda Doha.

“Ushahidi kama huo unaonyesha alikuwa katika kitendo cha kusafirisha dawa zinazobishaniwa kutoka Tanzania na inatosha kutengeneza kosa. Shahidi wa tatu anasema alipokata lile begi ndio walikuta paketi zile tatu zenye dawa,” alisema.

“Kwa kuegemea ushahidi huo, naona kabisa paketi zile ambazo baadaye zilithibitishwa kuwa na dawa za kulevya zilipatikana kutoka kwa mshtakiwa wa kwanza,” alieleza Jaji.

Kuhusu mshtakiwa wa pili, Jaji alisema maelezo yake ya kukiri kosa aliyoyaandika polisi, alieleza namna alivyoingia nchini Aprili 11, 2019 akiwa na msichana anaitwa Linda kwa dhamira mbili, moja kwa ajili ya kutalii na pili kufanya kazi ya dawa za kulevya.

Maelezo hayo yanasomeka “Pili ni kufanya kazi ya dawa za kulevya kusafirisha kutoka Tanzania kwenda sehemu ambayo ningepewa ujumbe wa wapi niyaache au kumpa mtu ambaye nitaagizwa. Mtu ambaye angenipa mzigo aliniambia nimsevu Prince Henry”.

Siku ya Aprili 17, 2019 walipigiwa simu washuke chini ya hoteli ambapo walikutana na mtu hawafahamu uraia wake, ambaye alimpa Linda mabegi mawili ambayo Linda angesafiri nayo na yeye (Martins) angepewa ya kwake siku atakapokuwa anasafiri.

“Nilipiga picha ya video ya yale mabegi, ili nimtumie mtu atakayeyapokea ili ajue mabegi yanafananaje. Kwenye saa 8:30 Linda alichukua teksi na nilimsindikiza hadi uwanja wa ndege tayari kuondoka. Baadaye nilirudi hotelini,” anaeleza katika maelezo hayo.

Jaji alisema kwa maelezo hayo, mshtakiwa wa pili anakiri kujihusisha na dawa za kulevya hapa Tanzania, kuyapeleka eneo lingine na kupokea maelekezo kutoka kwa mtu aliyemtaja kuwa ni Price Henry ili aweze kusafirisha dawa hizo za kulevya.

Kutokana na ushahidi huo, Jaji aliwatia hatiani washtakiwa hao kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya na kuwahukumu kifungo cha maisha jela magereza ya Tanzania.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live