Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dawa za kulevya sasa zasafirishwa kwa mananasi

70e3affa76a743ea20e1f70b71d3e36d Dawa za kulevya sasa zasafirishwa kwa mananasi

Thu, 24 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Kazi, Bunge, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama amesema serikali imebaini mbinu za usafirishaji dawa za kulevya ikiwemo ya kutumia mananasi.

Jenista alisema jana jijini Dodoma kuwa juhudi za udhibiti wa dawa za kulevya zimesababisha wimbi la watumiaji wa dawa tiba za viwandani zenye asili ya kulevya.

Aliyasema hayo jana alipotoa taarifa ya hali ya dawa za kulevya kwa mwaka 2020 ambayo aliwasilisha bungeni ikiwa ni kutekeleza sheria inayotaka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya iandae na kuiwasilisha bungeni taarifa ya hali ya dawa za kulevya nchini ya kila mwaka.

Jenista alisema moja ya changamoto katika vita hivyo ni kubadilika badilika kwa mbinu za kusafirisha dawa za kulevya na pia teknolojia inayotumika.

Alisema kutokana na udhibiti wa dawa za kulevya za viwandani zikiwemo heroin na cocaine, baadhi ya watumiaji walitumia dawa tiba zenye asili ya kulevya.

Alitaja mfano wa dawa hizo kuwa ni tramado, ketamini, valiamu na pethidini na kwamba matumizi ya dawa hizo bila kuzingatia ushauri wa daktari, ni hatari kwa kuwa husababisha uraibu na magonjwa ya mwili yakiwemo ya figo na ini.

Alisema utumiaji wa dawa hizo kwa kujistarehesha husababisha ukosefu wa dawa hizo kwa watu wanaozihitaji kwa tiba hivyo kusababisha usumbufu katika jamii.

Alisema serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya udhibiti kama vile Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Bohari ya Dawa, na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka ya kuuzia dawa na kampuni zinazojihusisha na uuzaji wa dawa.

Alisema mwaka jana serikali iliendelea kuongeza vituo vya matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya hadi kufikia vituo tisa kufikia Desemba mwaka jana na kutoa huduma ya tiba ya methadone bila malipo kwa waraibu 9,188.

Alisema vituo hivyo vipo katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Dodoma, Tanga na Pwani. Alisema serikali iliendelea kuratibu uanzishwaji na kusimamia uendeshwaji wa nyumba za upataji nafuu zinazoendeshwa na asasi za kiraia.

Alisema katika kipindi cha mwaka jana nyumba 31 zilitoa huduma hiyo katika mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Dodoma, Morogoro, Iringa, Mwanza, Kagera, Tabora na Arusha.

Vile vile, tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya iliendelea kutolewa katika idara za afya ya akili katika hospitali za Wilaya na Mikoa yote nchini ambapo waraibu 169,269 walipatiwa huduma ya tiba ya uraibu.

“Idadi kubwa ya waraibu walionekana kuathirika zaidi na matumizi ya vilevi kama vile pombe, bangi, mirungi, heroin na cocaine,” alisema na kuongeza kuwa matumizi na biashara ya dawa za kulevya ni tatizo linaloiathiri dunia licha ya jitihada za udhibiti zinazofanyika.

Aidha, Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya ya Dunia ya Mwaka 2020 inabainisha kuwa takribani watu milioni 269 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 64 walitumia dawa za kulevya mwaka 2018.

Jenista alisema bangi imeendelea kuwa dawa ya kulevya inayotumika zaidi duniani ambako kwa mwaka 2018 ilitumiwa na watu milioni 192. Alisema mwaka jana tani 13.23 za bangi zilikamatwa na kuhusisha jumla ya watuhumiwa 7,601.

Aidha, jumla ya mashamba ya bangi 28 yenye ukubwa wa ekari 26.2 yakihusisha watuhumiwa 34 yalikamatwa na kuteketezwa kwa mujibu wa sheria. Alisema tani 11.80 za mirungi zilikamatwa zikihusisha watuhumiwa 1,156.

Kiasi kikubwa cha mirungi iliyokuwa ilikuwa inasafirishwa kwa njia ya vifurushi kutoka Ethiopia kupitia Tanzania kwenda Amerika ya Kaskazini na Ulaya.

Aidha, katika kipindi hicho, jumla ya kilo 349.81 za heroin zilikamatwa nchini zikiwahusisha watuhumiwa 428 na kilo 4.52 za cocaine zilikamatwa zikiwahusisha watuhumiwa 80.

Chanzo: www.habarileo.co.tz