Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dar yatangaza vita na majambazi

C213a295f0bfca85f0f73013eb6aa233.png Dar yatangaza vita na majambazi

Wed, 26 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu mkoani humo wameanzisha kampeni kudhibiti majambazi.

Wakati Polisi ikiwataka majambazi wasalimishe silaha na kwamba haitakuwa na mzaha ikikutana nao sehemu yoyote, tayari imekamata watuhumiwa 20 wa makosa mbalimbali yakiwemo ya mauaji na ujambazi wa kutumia silaha.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Camillius Wambura katika taarifa yake alieleza kuwa Machi 18, mwaka huu saa 8:00 usiku Polisi walikamata watu watano wakituhumiwa kwa ujambazi.

Kamanda Wambura alisema watu hao walivamia katika nyumba ya Mkurugenzi wa Benki ya Azania, Mbweni Mpiji na kuwashambulia walinzi wa Kampuni ya Suma JKT na kupora silaha Short Gun Pump Action ikiwa na risasi tano.

Alieleza kuwa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam ilifuatilia na Mei 20, mwaka huu walikamata watuhumiwa hao na silaha. Kamanda Wambura alisema pia wanashikilia watu watano kwa tuhuma za mauaji.

Watuhumiwa hao ni Issa Karim maarufu Mdaka Bomu (33) mkazi wa Mbezi, Mohamed Juma maarufu Mabangi (31) mkazi wa Mbezi Mwisho, Selemani Seif maarufu Dullah Kishandu (34), mkazi wa Mbezi Mwisho, Samson Joseph maarufu Mjeuri (32), Mkazi wa Mbezi na Ezekiel Kennedy maarufu Simba MC, pia mkazi wa Mbezi.

Alisema Mei 8, mwaka huu saa 8:05 usiku maeneo ya Mikocheni A watuhumiwa hao wanadaiwa kuvamia katika baa ya Imbizo na kumshambulia kwa mapanga na marungu mlinzi, Regan Sylvester na kusababisha kifo chake papo hapo.

Aidha, watuhumiwa hao pia wanadaiwa kuhusika na tukio la unyang’anyi wa kutumia silaha Mabwepande ambako Mei 7, mwaka huu, saa 09:00 usiku walivamia katika kituo cha kuuzia mafuta cha Mexons na kuwashambulia walinzi, wahudumu na wateja na kupora Sh 440,000 na kisha kupora silaha aina ya Short Gun ya walinzi hao.

Pamoja na hayo, Kamanda Wambura alisema wamekamata watuhumiwa wanne wa wizi wa magari, na magari manne.

Watuhumiwa hao ni Babuelly Chao (43) mkazi wa Moshi, Sebastian Shembaru (36) mkazi wa Kigamboni, Hussein Misanya (33) mkazi Mabibo Relini na Said Rajabu (16) wa Mabibo. Wanatuhumiwa kuiiba magari maeneo ya Kinondoni na Ilala na walikamatwa na magari yenye namba za usajili T 817 ATQ Toyota Nadia, T 134 BPJ Toyota IST, T 952 CKB Toyota Mark II Grand na T 590 DTK Toyota IST.

Aidha, jeshi hilo limekamata pikipiki namba MC 136 CSA Boxer nyeusi iliyokuwa imeibwa Mei 15, mwaka huu maeneo ya Kibamba shule na kupelekwa Gairo mkoani Morogoro.

Kamanda Wambura alisema polisi walifanya ufuatiliaji na kuikamata pikipiki hiyo na kuirudisha Dar es Salaam.

Halikadhalika alisema Polisi inawashikilia watu watano kwa tyuhuma za kuvunja nyumba usiku na kuiba.

Alisema Mei 23, mwaka huu saa 08:30 usiku Mtaa wa Mikocheni A watuhumiwa hao wanadaiwa kuvunja nyumba ya Daud Ramadhani na kuiba vitu mbalimbali.

Alisema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na baadhi ya mali walizoiba ikiwamo televisheni moja aina ya LG inchi 55 ‘Flat screen’, simu mbili aina ya iphone, kompyuta mpakato mbili aina ya Dell na ‘mouse’ nne za kompyuta.

Aliwataja watuhumiwa ni Abeid Said almaarufu Gebe (41) mkazi wa Kinondoni, Laurent Mwazembe (44) wa Malamba Mawili, Ramadhani Mohamed (31) wa Mbezi, Julius Mapunda (34) wa Mbezi Njeteni na Emmanuel Zongo (30) wa Kigamboni.

Katika operesheni hiyo, alisema wanawashikilia watu sita kwa tuhuma za uvunjaji maduka usiku na kuiba. Aliwataja ni Kaburu Mohamed (30) wa Buza Kanisani, Iddi Ally (30) wa Tandika, Said Ramadhani (33) wa Kitunda, Lucas Danford (31) wa Buguruni, Shaban Bakari (33) wa Tandika Kaburi Moja na Khamis Bahati (38) wa Buza kwa Mama Kibonge.

“Watuhumiwa hawa wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya uvunjaji maduka nyakati za usiku katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam hususani katika mitaa ya Kariakoo na Ukonga Banana,” alisema.

Kamanda Wambura aliwaambia wanahabari, “Yani hapa ni shoo kwa shoo hakuna msalia mtume, kamwe mhalifu hawezi kushindana na Jeshi la Polisi na tena kwa kuwaonesha tumejipanga wafanya ujambazi waone shoo tutakayowapa,”

Aliongeza, “Wewe kama unayo silaha na tukakukuta nayo nyumbani au mahala popote pale ina maana wewe ni mhalifu ambaye ni mpiganaji na iweje tukuache, hakika hatapona mtu tena wakae chonjo ni saa mbaya.”

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Amos Makalla aliagiza Jeshi la Polisi kuwanyang’anya silaha majambazi na hakuna muda wa kuwabembeleza.

“Hawa majambazi wamebeep na ninawaagiza askari kuhakikisha kuwa wanawashughulikia kwa kila namna yani shoo kwa shoo hakuna kulemba…nataka mkawaoneshe shoo hawa majambazi, nasisitiza hakuna kona kona yani ni kuwashughulikia tu.”

“Sina wasiwasi na Jeshi la Polisi kwanza ninaamini kuwa kazi mnaiweza na hawa majambazi wanatujaribu wameona Mkuu wa Mkoa mpya na hata wewe Mkuu wa Polisi wa Kanda Maalumu na kwa sasa ndiyo wanaona ni muda wa kutujaribu, sasa ninaagiza kazi ikafanyike,” alisisitiza Makalla.

Hivi karibuni katika hotuba zake mara kwa mara, Rais Samia Suluhu Hassan amekemea vitendo vya ujambazi na uhalifu alioiuta kuwa unapima kina cha maji cha serikali yake akitaka hatua za kuudhibiti zichukuliwe mara moja.

Chanzo: www.habarileo.co.tz