Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dar yajipanga kupambana na ‘Panya Road’

Panyaroad Darrrr Mmoja wa waathirika wa panya road

Sun, 1 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kufuatia matukio ya uporaji yanayofanywa na vijana wanaojulikana kwa jina la Panya Road jijini hapa, baadhi ya wakazi wameweka mikakati ya kupambana nao.

Juzi vijana hao walisababisha taharuki baada ya kuwajeruhi watu 23 na kuwapora fedha, simu na vifaa vya kielektroniki, zikiwemo televisheni katika maeneo ya Chanika na Tabata jijini hapa.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari juzi alisema wanawashikilia vijana 10 kuhusiana na tukio hilo, huku wakiendelea kuwatafuta wengine.

Akizungumza na Mwananchi jana Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija alisema tayari ameshatoa maelekezo kwa wenyeviti wa Serikali za mitaa isiyokuwa na vikundi shirikishi kuanzisha mara moja.

Ludigija alisema kuna mitaa imejisahau, hasa kwenye suala zima ulinzi shirikishi, jambo linalosababisha watu wasiokuwa waaminifu kufanya uhalifu.

Related ‘Panya Road’ gumzo DarAdvertisement “Kuna mitaa haina ulinzi shirikishi, nimewaagiza wenyeviti wa mitaa ambao ndio wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama kwenye mitaa yao kuuanzisha mara moja.

“Tuna vituo vidogo vya polisi, vituo hivi haviwezi kukaa na askari kwa saa 24, na pia hawawezi kufanya doria kwenye kila eneo, ndio maana tumeelekeza ni lazima kila eneo liwe na ulinzi shirikishi,” alisema.

Alisema kamati ya ulinzi na usalama imeshaanzisha msako kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na wananchi ili kubaini vijana wanaojihusisha na vitendo hivyo.

“Wapo vijana waliokamatwa wanaendelea kutupa ushirikiano vizuri, na vikundi hivi vya kihalifu vinatoka maeneo mbalimbali, lakini pia wamekuwa wakishirikiana na wenyeji wa maeneo husika,” alisema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo ametoa siku saba ndani ya wilaya hiyo maeneo yote yawe yameanzisha polisi jamii ili kukabiliana na vitendo vya uhalifu.

Jokate aliyasema hayo jana, katika kikao kazi kilichowakutanisha Jeshi la Polisi, viongozi na wenyeviti wote wa Serikali za mitaa katika wilaya hiyo ambapo kwa sehemu kubwa wamehimizwa kushiriki kikamilifu katika suala la ulinzi, ikiwa pamoja na kuanzisha polisi jamii.

Alisema wenyeviti wote wa Serikali za mitaa ndani ya wilaya hiyo wanatakiwa kuhakikisha wanaanzisha polisi jamii ili kukabiliana na vitendo vya kihalifu vinavyotokea kwenye mitaa yao.

“Wenyeviti wa Serikali za mitaa mlioko kwenye kikao hiki hamko hapa kwa bahati mbaya, bali mmetajwa kwenye Katiba, kwenye Ilani ya CCM, katika sheria ndogo ya Manispaa ya Temeke na katika Sheria ya Serikali za mitaa. Hivyo ni wajibu wetu kushiriki katika ulinzi kwenye maeneo tunayotoka,” alisema Mwegelo.

Katika hatua nyingine, baadhi ya wakazi wa Tabata Kisiwani na Twiga walifanya kikao kilichohudhuriwa na Mkuu wa Polisi Kituo cha Tabata, Oraity Shomari kujadili usalama, ikiwemo kutaja majina ya vijana wanaojihusisha na vikundi hivyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live