Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dar: Watu 11 wahukumiwa kunyongwa kwa mauaji ya Lotter

Derek Lotter Derek Lotter enzi za uhai wake

Fri, 2 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imewahukumu kunyongwa hadi kufa washtakiwa 11 katika kesi ya mauaji ya mwanaharakati wa ujangili, raia wa Afrika Kusini, Wayne Derek Lotter.

Katika hukumu yake iliyosomwa leo Ijumaa, Desemba 2, 2022 na Jaji Laila Mgonya imewatia hatiani washtakiwa hao baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa mashtaka kupitia mashahidi wake 32 kuwa umethibitisha mashtaka dhidi yao bila kuacha mashaka yoyote.

Waliotiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu hiyo ni pamoja na Rahma Almas, mkazi wa Mbagala B, Nduimana Ogiste, maarufu kama mchungaji na raia wa Burundi, Godfrey Salamba mkazi wa Kinondoni Msisiri A na Chambie Juma Ally, mkazi wa Kia/Boma.

Wengine ni Allan Elikana Mafue; Ismail Issah Mohammed (Machipsi); Leornad Phillipo Makoi; Ayoub Selemani Kiholi; Abuu Omary Mkingie na Habonimanda Augustine Nyandwi (pia raia wa Burundi) na Michael Dauv Kwavava;

Lotter ambaye alikuwa Mkurugenzi na Mwanzilishi-mwenza wa Shirika silo la kiserikali la PALMS Foundation, lililokuwa linahusisha na mapambano ya ujangili.

Mwanaharakati huyo aliuawa Agosti 16, 2017 kwa kupigwa risasi na watu waliomvamia akiwa kwenye teksii yeye na mwenzake, katika makutano ya barabara za Chole na Haile Selaissie, Masaki wilayani Kinondoni.

Awali washtakiwa katika kesi hiyo ni 22, wakiwemo raia wa Burundi wawili.

Hata hiyo baada ya kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa usikilizwaji kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu iliyofunguliwa katika hatua ya uchunguzi wa awali kwa ajili ya kukamilisha taratibu za washtakiwa wanne walifutuwa kesi na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wakabakia 11 ambao wote wametiwa hatiani.

Baada ya mahakama kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka iliwaachia huru washtakiwa wengine Saba baada ya kuridhika kuwa hawakuwa na kesi ya kujibu.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 13 ya mwaka 2021 washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka mawili, kula njama kumuu Lotter na kumuua kwa maksudi Lotter.

Wametiwa hatiani Kwa makosa hayo yote kutokana na ushahidi wa mashahidi hao na vilelezo mbalimbali yakiwemo maelezo yao ya onyo waliyoyatoa wakihojiwa Polisi ambayo pia yameungwa mkono na ushahidi mwingine kama sheria inavyoelekeza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live