Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Daktari mbaroni wizi wa vifaa vya ujenzi wa hospitali

Mbaroni Daktari mbaroni wizi wa vifaa vya ujenzi wa hospitali

Fri, 9 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu wanne wakiwamo watumishi wawili wa Serikali na mlinzi wamekamatwa kwa tuhuma za wizi wa vifaa vya ujenzi katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe.

Taarifa za wizi huo zimetolewa leo Februari 9, 2024 na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Butusyo Mwambelo alipozungumza na Mwananchi Digital.

Amesema wizi wa vifaa hivyo unadaiwa kutokea jioni ya Januari 31, 2024.

Amesema waliokamatwa ni na daktari aliyekabidhiwa funguo za stoo, na mtunza stoo ambaye alikabidhiwa kutunza vifaa hivyo vya ujenzi.

Kaimu kamanda amesema pia mlinzi aliyekamatwa baada ya kupekuliwa nyumbani kwake alikutwa na vifaa vingine vya hospitali hiyo.

"Kweli tukio la wizi limetokea likafunguliwa jalada la uchunguzi na mkurugenzi kuunda kamati ya ufuatiliaji wa jambo hilo, ikaonekana vifaa vya ujenzi na umeme vimeibiwa," amesema Mwambelo.

Mganga mkuu wa halmashauri ya mji wa Makambako, Dk Alexander Mchome amethibitisha kutokea wizi huo na kudai upo utaratibu wa kutoa taarifa na anayeruhusu kuzitoa ni mkurugenzi wa halmashauri.

"Unatakiwa kuandika barua, akiridhia basi anayehusika kutoa taarifa hizo atakupa, tukio lipo ila wasiliana na ofisi ya mkurugenzi akiruhusu tutakusaidia," amesema Mchome alipoulizwa taarifa zaidi kuhusiana na tuhuma hizo na mwandishi wa habari hii.

Diwani wa kata ya Mlowa, Odilo Fute amekiri kuwa vifaa hivyo vimeibiwa lakini jambo hilo lipo kwenye vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

"Taarifa hizi nimezipata ilikuwa Ijumaa kwamba kuwa tukio limetokea kuna vitu vimeibiwa na kwa maelezo milango haijavunjwa ni kama kuna watu wamefungua na kutoa vitu ndani," amesema Fute.

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Mlowa, Hangaika Ngohonzela amesema tukio hilo limekuwa la siri zaidi kwani kama wananchi wamehusika taarifa zingetoka siku hiyohiyo.

"Lazima uchunguzi ufanyike kwani kama hospitali haijavunjwa na vitu havipo na wenyewe wapo hapo inawezekana ni wataalamu ambao wanajua kwamba pale kuna moja, mbili, tatu ndiyo maana hili jambo lipo kwa siri zaidi," amesema Ngohonzela.

Baadhi ya wananchi, wakiwamo Jackson Mlelwa na Ezekia Chongolo wamesema haileti taswira njema kuona Serikali inanunua vifaa kwa ajili ya wananchi lakini baadhi ya watu walioaminiwa wanafanya vitendo visivyofaa vya kuihujumu.

Wameiomba Serikali kuchunguza kwa makini tuhuma za wizi wa vifaa hivyo vya ujenzi ili kubaini wahusika na kuchukuliwa hatua stahiki.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live