Mtumishi katika Hospitali ya Rufani Mkoa wa Kitete Tabora, Dk. Festo Jafari, ambaye ni mmiliki wa Zahanati ya Hossiana Mission katika Manispaa ya Tabora, ameingia matatani baada ya kubainika kuwarubuni wagonjwa wanaopewa rufani kwenda hospitali kubwa na kuwapatia huduma katika zahanati yake kinyume na miongozo ya afya.
Kutokana na madai hayo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paulo Chacha, alifika katika zahanati hiyo juzi na kuliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata mkurugenzi mwenza wa zahanati, Sara Elius, Mganga Mfawidhi wa Zahanati na Ezra Masesu kwa tuhuma za kurubuni wagonjwa wanaopewa rufani.
Pia aliagiza mganga mstaafu ambaye jina lake halikutajwa anayedaiwa kuhusika kutoa huduma hizo na mmiliki wa zahanati hiyo, Dk. Jafari ambaye pia mtumishi katika Hospitali ya Kitete.
Chacha alitoa maagizo hayo baada ya zahanati hiyo kubainika kurubuni wagonjwa wanaotakiwa kupata huduma za kibingwa katika Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Bugando jijini Mwanza na kuwalaza kwa zaidi ya siku tatu pamoja na kuwafanyia huduma za upasuaji kinyume cha taratibu.
“Kamateni wote mtachambua kwa makini ni nani anayetakiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka kati yao. Pia Katibu Tawala wa Mkoa waandikie barua Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC) kwa ajili ya kuwachukulia hatua wahudumu wote wa afya watakaobainika kuhusika kwenye tukio hili,” alisema Chacha.
Inadaiwa kuwa wagonjwa waliokuwa wakipewa rufani kutoka Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Tabora ya Kitete, kwenda katika hospitali kubwa ikiwamo Bugando, walikuwa wanarubuniwa na mmiliki wa zahanati hiyo kisha kuwafanyia matibabu kinyemela katika zahanati yake.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk. Honoratha Rutatinisibwa, alieleza walivyobaini tukio hilo na athari zake kwamba mgonjwa mmoja, kijana wa miaka 24, alikuwa na tatizo la kuvunjika mfupa wa paja, hivyo alitakiwa akapate huduma za kibingwa lakini wakashangaa kukuta amelazwa kwenye zahanati hiyo.
“Alipewa rufani akamwone daktari bingwa wa mifupa Bugando lakini tukashangaa amelazwa hapa wanampa huduma ambayo si stahiki. Kwa hiyo wangeweza kusababisha madhara kwa huyo mgonjwa,” Dk. Rutatinisibwa.
Katika hatua nyingine, Chacha aliagiza zahanati hiyo kufungwa kupisha taratibu za kiuchunguzi pamoja na taratibu za kisheria kwa mujibu wa miongozo ya afya.