Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Daktari atoa ushahidi kesi ya Mbowe na wenzake, ataja kitu cha ncha kali

65105 Pic+mbowe

Tue, 2 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar Es Salaam. Shahidi wa tano katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa chama kikuu cha upinzani Tanzania cha Chadema, akiwemo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa askari waliojeruhiwa katika maandamano ya Chadema, walipigwa na kitu chenye ncha kali na butu.

Shahidi huyo, Dk Juma Khalfani (54), ambaye ni daktari Msaidizi kutoka Hospitali Kuu ya Jeshi la  Polisi, Kilwa Road nchini Tanzania ameieleza hayo leo Jumatatu Julai Mosi, 2019 wakati akitoa ushahidi wake katika Mahakama hiyo iliyopo Dar Es Salaam Tanzania.

Akiongozwa na wakili wa Serikali, Salim Msemo, mbele ya hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, Dk Khalfani amedai majeruhi hao ambao ni PC Fikiri Mtega na Koplo Rahim Msangi, walifikishwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya matibabu baada ya kujeruhiwa katika maandamano yanayodaiwa kuwa ni ya wafuasi wa Chadema, eneo la Mwananyamala.

Dk Khalfani ambaye pia ni Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la  Polisi , amedai kuwa Februari 16, 2018, majira ya saa 5:40 usiku, akiwa katika wodi ya wazazi, alipewa taarifa na nesi kutoka chumba cha wagonjwa wa dharura kuwa kuna wagonjwa wawili wamefikishwa katika hospitali hiyo huku hali zao zikiwa sio nzuri.

"Nikiwa natekeleza majukumu yangu kama daktari wa zamu katika wodi ya wazazi, usiku ule alikuja nesi kutoka chumba cha wagonjwa wa dharura na kuniambia kuwa kuna wagonjwa wawili wameletwa na hali zao sio nzuri" amedai Dk Khalfani.

Amedai baada ya kupewa taarifa hiyo alichukua uamuzi wa kwenda chumba cha wagonjwa wa dharura na kuwakuta wagonjwa na kwamba alimuuliza Nesi kama wagonjwa hao wamepatiwa huduma ya kwanza.

Pia Soma

"Nesi aliniambia hawajapatiwa huduma ya kwanza na mimi niliwaelekeza manesi wawachome sindano ya kutuliza maumivu kabla ya kuendelea na hatua nyingine za matibabu," amedai Shahidi.

Dk Khalfani amedai majibu ya vipimo vya Koplo Rahimu yalionyesha kuwa alijeruhiwa na kwa kupigwa na kitu chenye  ncha kali  shingoni na kichwani, wakati PC Fikiri Mgeta, yeye alionekana amejeruhiwa na kitu kinachofanana na tufe au butu.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mbunge waTarime Mjini Esther Matiko;   Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa; Naibu Katibu Mkuu Taifa, Zanzibar, Salum Mwalimu;  Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; Mbunge wa Kawe,  Halima Mdee, Mbunge wa Tarime vijijini, John Heche, mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vicent Mashinji.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa 13 likiwemo la kula njama, ambapo wote wanadaiwa kuwa, February 1 na 16, 2018, Dar es Salaam waliku?a njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.

Chanzo: mwananchi.co.tz