Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Daktari anayedaiwa kutoa mimba wagonjwa, asomewa kesi ya uhujumu uchumi

90133 Daktari+pic Daktari anayedaiwa kutoa mimba wagonjwa, asomewa kesi ya uhujumu uchumi

Sat, 28 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam . Daktari, Awadhi Juma (40) kutoka Hospitali binafsi ya Dental Clinic, iliyopo Sinza Mori, Dar es Salaam na muuguzi mmoja, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka saba likiwamo la kutoa mimba wagonjwa na kutakatisha fedha kiasi cha Sh260,000.

Mbali na Juma, ambaye ni mkazi wa Kunduchi Salasala, mshtakiwa wa pili ni Kidawa Ramadhani (26) ambaye ni muuguzi na mkazi wa Manzese.

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo Ijumaa Desemba 27, 2019 na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi, Vicky Mwaikambo.

Kabla ya kusomewa mashtaka yao, Mwaikambo amesema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kutokana na Mahakama ya Kisutu kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu kutoka kwa DPP.

Akiwasomea hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon akisaidiana na Glory Mwenda, amedai washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba  139/2019.

Miongoni mwa mashtaka hayo, Simon amedai, katika tarehe tofauti Oktoba 2019 eneo la Sinza Mori, jijini Dar es Salaam, washitakiwa hao wakiwa na lengo la kutoa mimba mgonjwa, waliingiza bomba la sindano katika uke wa mgonjwa F.R na S.S na kusababisha kuharibika kwa mimba.

Pia, katika tarehe tofauti, Agosti 2002, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Juma kwa lengo la kudanganya, alighushi cheti cha Diploma cha Utaalam wa tiba ya Kinywa akionesha ni halali na kimetolewa na  chuo cha tiba cha Muhimbili wakati akijua si kweli.

Katika shtaka la kutakatisha fedha, Juma anadaiwa  kati ya Mei 2015 na Desemba 4, 2019  alijipatia Sh 260,000  wakati akijua fedha hizo ni zao la kosa la jinai la kugushi.

Simon alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na Hakimu Mwaikambo, aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 10, 2020 itakapotajwa.

Washitakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Chanzo: mwananchi.co.tz