Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Daktari aieleza alivyogundua Ukimwi kwa mtoto aliyebakwa

49128 Mtoto+pic

Thu, 28 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Daktari wa Hospitali ya Rufaa ya Amana, Godfrey Kamani (38) ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Ilala jinsi alivyomfanyia uchunguzi mtoto wa kike anayedaiwa kubakwa na kubaini ana maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na magonjwa ya zinaa.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 181 ya mwaka 2018, Simon Zacharia (45) mkazi wa Mwanagati, anadaiwa kumbaka mtoto huyo wa kike mwenye umri wa miaka 14.

Akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi, Adolf Sachore na Wakili wa Serikali, Grace Mwanga katika kesi hiyo, shahidi huyo wa upande wa mashtaka alisema amefanya kazi katika hospitali hiyo kwa miaka saba katika kitengo cha magonjwa ya kina mama na awali alikuwa katika kitengo cha dharura na magonjwa ya nje.

Alidai kuwa Februari 27, mwaka jana nyakati za mchana akiwa katika majukumu yake ya kawaida, aliitwa kumuona mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 ambaye alikuwa ameambatana na mama yake na kwamba ambao waliingia katika chumba chake cha matibabu.

Aliieleza Mahakama kuwa mama wa mtoto huyo alimpatia taarifa kuwa binti yake huyo alitoroka nyumbani na kwamba alikuwa akiishi na mwanamume kama mke na kwamba alikuwa na fomu ya polisi namba tatu (PF3).

Dk Kamani alieleza kuwa mtoto huyo hakuweza kujieleza na yeye hakuwa na namna ya kumlazimisha kuongea, hivyo ilimlazimu kuchukua maelezo ya mama yake na kumfanyia uchunguzi.

Alieleza kuwa uchunguzi alioufanya ulionyesha kuwa hakuwa na bikra, ana maambukizi ya HIV na pia ana magonjwa ya zinaa hivyo aliijaza PF3 siku hiyohiyo na kumpatia matibabu.

Baada ya kutolewa kwa ushahidi huo, mshtakiwa Zacharia alimuuliza swali shahidi huyo kwamba linapotokea tatizo kama hilo mshtakiwa naye hapaswi kupimwa?

Akijibu swali hilo, Dk Kamani alisema kwa mujibu wa kazi yake, anahusika na wale wanaokwenda hospitali na kwamba wanamfanyia vipimo na kutoa maelezo kwa kile wanachokiona.



Chanzo: mwananchi.co.tz