Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DPP kuamua hatma hausiboi aliyeua familia Dar  

449fbb8ab6ec7625bae7b0c6a9b14978.jpeg DPP kuamua hatma hausiboi aliyeua familia Dar  

Thu, 15 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

JESHi la Polisi Mkoa wa Kinondon limesema upelelezi kuhusu mauaji ya mama na watoto wake wawili wa kike umekamilika na faili limepelekwa Ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP) kwa hatua zaidi.

Ilidaiwa kuwa Emilly Mutaboyerwa na binti zake Damita (13) na Daniela Mutaboyerwa (15), waliuawa Juni 9, mwaka huu na miili ilikutwa Juni 11 nyumbani kwao Mtaa wa Maryknol, Masaki wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.

Polisi walimkamata Shadrack Kapanga (34) akituhumiwa kufanya mauaji hayo akiwa ni mfanyakazi wa ndani katika familia hiyo.

Imefahamika kuwa Kapanga ni mtuhumiwa namba moja katika shauri hilo na pia polisi walimkamata aliyedaiwa kuwa alikuwa mpenzi wa Emily na hadi sasa wapo rumande.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Ramadhani Kingai alisema upelelezi umekamilika na jalada la kesi lipo kwa DPP.

“Jeshi la Polisi Kinondoni limeshakamilisha kazi ya uchunguzi wa sakata hili la mauaji na kwa upande wetu kama ilivyo kawaida tukishawasilisha faili kwa ofisi ya DPP tunangojea kama kunakuwa na maelekezo mengine,” alisema Kamanda Kingai.

Aliongeza, “Kama likiwa sawa kwa maana ya upelelezi umekamilika inabakia suala la kupelekwa mahakamani kwa watuhumiwa na kuanza kwa kesi, kwa sasa bado tunawashikilia watuhumiwa hawa na wapo wawili aliyekuwa mfanyakazi na aliyekuwa mpenzi wa mama wa watoto wale waliouawa.”

Kuhusu watu wangapi walihojiwa, Kamanda Kinai alisema suala hilo hawezi kulizungumzia, lakini akasema watu wawili walikamatwa ila wapo wengine waliohojiwa.

Kapanga alikutwa akiuza simu za marehemu, televisheni, kisimbuzi cha DSTV na rimoti na alidaiwa alikuwa katika jitihada za kutoroka.

Kamanda Kingai pia alisema Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea kukabili matukio ya uhalifu na kwa siku za hivi karibuni eneo la Mabwepande kuna watuhumiwa wa ujambazi wamekamatwa wakijaribu kuvamia nyumba.

“Operesheni imekuwa ikiendelea kwa hali na mali ya kusaka wezi na majambazi na kwa hivi majuzi wamekamatwa majambazi wakitaka kuvamia na kuiba kwenye nyumba moja, kwa sasa tunaendelea na kukabiliana na wezi katika maeneo mengine, hali ya usalama siyo mbaya kwa kuwa matukio makubwa ya ujambazi yamedhibitiwa,” alisema.

Kuhusu biashara ya dawa za kulevya na uuzaji wa miili, Kamanda Kingai alisema wamefanikiwa kudhibiti uuzwaji wa dawa za kulevya na kuitaka jamii kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi dhidi ya matukio hayo.

Akizungumzia biashara ya uuzaji wa miili, alisema bado jamii ina wajibu wa kushiriki kukabiliana na biashara hiyo huku akiweka wazi kuwa Polisi imekuwa likiendelea na operesheni za mara kwa mara.

Chanzo: www.habarileo.co.tz