Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DPP awatangazia kiama waliopanda mbegu Deci

56619 Pic+dpp

Fri, 10 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga amewagongea kengele ya tahadhari akiwaonya waliokuwa wanachama wa kampuni ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (Deci) iliyokuwa inajishughulisha na upatu dhidi ya zahma itakayowakuta watakaojitokeza kudai fedha zao walizowekeza.

Mganga alitangaza tahadhari hiyo dhidi ya washirika hao wa Deci siku mbili baada ya Mahakama Kuu kuamuru mali za kampuni hiyo zikiwamo Sh14.1 bilioni taslimu kutaifishwa, kufuatia wakurugenzi wake kutiwa hatiani kwa kosa la kuendesha shughuli za upatu.

Wanachama hao waliwekeza fedha katika kampuni hiyo kwa viwango tofautitofauti kwa kucheza upatu, ili baadaye wapate fedha nyingi kwa muda mfupi, utaratibu uliojulikana kupanda mbegu kisha kuvuna.

Akizungumza na Mwananchi juzi kuhusu hatima ya wanachama hao waliopanda mbegu zao ambao wengi walikwa hawajavuna, Mganga alisema anawasubiri wajitokeze kudai ili awashughulikie kwani kushiriki upatu ni kosa la jinai na kila atakayejitokeza kudai ataishia kortini.

Alisema walioendesha shughuli za upatu na waliocheza wote walikuwa wakitenda kosa la jinai, lakini wakati wakurugenzi wa Deci wanashtakiwa hawakuweza kushtakiwa wote na walioshiriki kucheza kutokana na changamoto ya uwingi wao.

“Lakini sasa hivi atakayekuwa anajitokeza anataka kuja kudai hizo, namkamata, twende. Si wewe umejileta mwenyewe umecheza upatu, twende tukasemezane vizuri ni kwa nini umecheza upatu,” alisema.

Wakati akitoa tahadhari hiyo dhidi ya wapanda mbegu hao wa Deci, tayari wanachama sita ambao ni miongoni mwa waliopanda mbegu walishakamatwa na kuhojiwa polisi kabla ya kuachiwa kwa dhamana.

Wanachama hao Andrew Tungaraza, Frida Msuva, Imelda Adolph, Jackson Nyera, Tadea Mgoso na Philemon Mwarkowalitiwa mbaroni Aprili mosi wakiwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, baada kuwasilisha maombi wakiomba kuunganishwa katika maombi ya DPP ya kutaifisha mali za Deci.

Katika maombi hayo hao waliokamatwa pamoja na wenzao wengine 12 walikuwa wakidai kuwa wao ni miongoni mwa wa wanachama wa Deci waliokuwa wamepanda mbegu zao kwa viwango tofautitofauti huku wengine wakiwa wameshapata sehemu ya mavuno na wengine wakiwa bado kabisa.

Hivyo walikuwa wanaomba wote kwa pamoja walipwe jumla ya Sh2.4 bilioni katika fedha hizo ambazo DPP alikuwa anaomba mahakama iamuru zitaifishwe na kuwa mali ya Serikali.

Siku hiyo baada ya kutoka tu mahakamani walitiwa mbaroni na kisha kufikishwa katika kituo kikuu cha Polisi Dar es Salaam, ambako walihojiwa kisha wakaachiwa kwa dhamaba.

Hata hivyo baadaye mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi yao ya kutaka kuunganishwa katika maombi ya DPP, kutokana na kasoro za kisheria katika hati ya kiapo kilichokuwa kinaunga mkono maombi yao.

Kuhusu hatua dhidi yao hao ambao tayari walishakamatwa na kuhojiwa DPP alisema kuwa bado wanaendelea na ushahidi dhidi yao lakini akaseema kwa hao kuna mambo mawili ama kuwashtaki au anaweza akaamuja kutokuwashtaki kwani bado kuna mambo fulani muhimu anayaangalia.

Viongozi hao wa DECI, ambao walikuwa wachungaji, viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Kipentekosti, walitiwa hatiani kwa kosa hilo mwaka 2013 na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya jumla ya Sh21 milioni. Walilipa faini hiyo na hivyo wakaepuka kifungo.

Waliotiwa hatiani katika kesi hiyo, ambao ndio wajibu maombi katika maombi ya DPP ni Jackson Sifael Mtares, Dominick Kigendi, Timotheo Saigaran ole Loitginye na Samwel Sifael Mtares.



Chanzo: mwananchi.co.tz