Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP), Biswalo Mganga amewataka watu wote waliofanyiwa vitendo vya udhalilishaji ikiwemo kubakwa au kuingiliwa kinyume na maumbile kujitokeza na kutoa taarifa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Agosti 26,2019 jijini Dar es Salaam, amesema hivi karibuni amejitokeza mtu (jina tunahifadhi) ambaye amekuwa akitumia majina tofautitofauti na kufanya vitendo vya udhalilishaji.
Amesema amekuwa akienda hoteli mbalimbali na kuwawekea wakina dada dawa kisha kuwabaka na kuwaingilia kinyume na maumbile kisha kuwaibia.
"Mara ya kwanza tulimfungulia mashtaka Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni na kisha kuwekewa dhamana lakini baada ya kutoka aliendelea na vitendo vilevile," amesema Mganga
Amesema tayari wameshafuta kesi iliyokuwa Mahakama ya Kinondoni kisha kumfungulia kesi nyingine mbalimbali Agosti 21, katika Mahakama ya Kisutu ikiwemo ya uhujumu uchumi.
"Hakuna haki isiyokuwa na mipaka lazima kuangalia mtu kaathirika vipi wapo wengi hapa Dar es Salaam waliofanyiwa vitendo hivyo wakiwemo wake za watu," amesema
Pia Soma
- Waziri Mkuu Sudan apunguza bajeti ya jeshi
- Jinsi Jaji alivyoyatupilia mbali mapingamizi ya Serikali ya Tanzania dhidi ya Tundu Lissu
- Waziri Ummy atoa somo kwa chama kipya cha Urembo na Vipodozi Tanzania
Aidha Mganga amewataka watu kufuata sheria kwa kuwa amani na utulivu ni jukumu la kila mmoja.