Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DPP atoa neno wanaobainika kujipatia mali kinyume cha sheria

29169 Jaji+pic TanzaniaWeb

Wed, 28 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Mkurugenzi wa mashtaka nchini, Biswalo Mganga amesema Serikali itakuwa ikichukua mali za watuhumiwa waliotiwa hatiani ili wasitumie baada ya kumaliza adhabu walizopewa na Mahakama.

Akizungumza leo Jumanne Novemba 27, 2018 kwenye mkutano ulioandaliwa na taasisi ya Wayamo Foundation kuwajengea uwezo waendesha mashtaka na majaji  kutoka nchi za Afrika Mashariki wa kukabiliana na uhalifu wa kimataifa.

"Kumekuwa na tabia baadhi ya wahalifu waliojipatia mali kwa njia haramu wanapokamatwa na kufungwa kwa mujibu wa sheria wakishamaliza vifungo vyao wanatumia utajiri walioupata kwa njia zisizo halali, hivyo tutakuwa tukirejesha hizo mali kwa umma," amesema Mganga.

Amesema katika ulimwengu wa sasa wahalifu hawana mipaka ya kijiografia jambo ambalo watekelezaji wa sheria wameona kuna umuhimu wa kubadilishana taarifa za upelelezi na kuwachukulia hatua wahalifu.

Awali, Jaji Mkuu mstaafu Tanzania, Mohamed Chande Othman wakati akifungua mkutano huo amesema ushirikiano katika kanda ya Afrika Mashariki utasaidia kukabiliana na uhalifu wa kimataifa.

Amesema takwimu zinaonyesha Tanzania imekuwa ikitumiwa na magenge ya wafanyabiashara ya kusafirisha binadamu kwa njia haramu hivyo upo umuhimu wa kushirikiana kukomesha vitendo hivyo.

"Kwa mwaka wahalifu wanapitisha watu 12,000 hapa nchini kuelekea Msumbiji hadi Afrika Kusini mkutano huu una nafasi muhimu ya kuwawezesha wadau kushirikiana kukabiliana nao,” amesema Jaji Othman.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa taasisi ya Wayamo Foundation, Bettina Ambach amesema taasisi hiyo inajivunia mabadiliko katika mifumo ya kisheria katika nchi wanazotoa mafunzo hayo.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz