Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DPP atoa kauli hatma ya Sethi

Dpppic Data Harbinder Sethi

Fri, 10 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) ameeleza hatima ya Mfanyabiashara Harbinder Sethi baada ya kuibuka utata wa kisheria kuhusu umiliki wa mitambo ya Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) aliyotumia kuweka dhamana.

Sethi aliachiwa huru Juni 16, mwaka huu baada ya makubaliano yake na DPP kumaliza kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa inamkabili.

Katika makubaliano yake ya kuachiwa huru, Sethi alikiri makosa yake na kukubali kulipa faini ya Sh200 milioni ambazo alizilipa palepale na fidia ya Sh26.9 bilioni alizotakiwa kuzilipa kwa utaratibu maalumu baada ya kuweka dhamana mitambo ya IPTL.

Hadi hivi karibuni, mitambo hiyo ilikuwa chini ya umiliki wa Kampuni ya Pan Africa Power Solution (T) Limited (PAP) inayomilikiwa na Sethi, lakini hukumu ya hivi karibuni ya Mahakama ya Rufani iliyobatilisha ununuzi wa kampuni ya IPTL kwa PAP, ikiwemo mitambo hiyo, iliibua maswali mengi likiwemo la hatima na uhalali wa dhamana ya Sethi aliyetumia mitambo hiyo.

Akizungumzia suala hilo juzi, DPP Sylvester Mwakitalu aliliambia Mwananchi kuwa uamuzi huo wa mahakama hautaathiri makubaliano ambayo Serikali ilifikia na Sethi.

Mwakitalu alifafanua kuwa masharti ya kuachiwa huru kwa Sethi ni kulipa fidia kama walivyokubaliana na kuidhinishwa na mahakama.

Advertisement Alisema mfanyabiashara huyo akishindwa kulipa fidia ndani ya muda waliokubaliana (miezi 12) watamkamata na kumrudishia mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.

“Kwanza kwenye makubaliano tuliyoingia na Sethi, yeye anatakiwa kulipa fedha na kuna schedule (ratiba) ya malipo ambayo tuliiweka. Akishindwa kulipa makubaliano yetu yanatutaka tumrudishie mashtaka na tuendelee na kesi. Muda wake wa kulipa bado haujaisha.

“Kwa hiyo, sisi hatuko-concerned (hatuhangaiki) sana na maamuzi hayo unayoya-refer (unayoyarejea). Sisi tunaamini atatekeleza makubaliano, akishindwa kutekeleza, basi kuna remedy (tiba) ambazo ziko kwenye mkataba wetu. Moja ni kurudisha yale mashtaka na kuendelea na kesi.

“Bahati nzuri ni kwamba kabla ya kuingia kwenye plea-bargain (majadiliano ya kukiri kosa), sheria inatutaka tumuoneshe ushahidi tulio nao dhidi ya makosa yanayomkabili. Kwa hiyo tulimuonyesha na tuna ushahidi wa kutosha,” alisema Mwakitalu.

Alifafanua kuwa mshtakiwa akiridhika anakuwa na hiyari kuamua kesi iishie hapo kwa yeye kukiri kosa kwa kuzingatia kwamba upande wa mashtaka unayaondoa baadhi ya makosa, au aende kwenye usikilizwaji kamili wa kesi.

“Kwa hiyo, kwetu sisi whether (kama) kuna maamuzi ya mahakama nyingine kuhusiana na mitambo ya IPTL au la, kwetu siyo issue (jambo) kubwa kwa sababu sisi hatukuishtaki IPTL, sisi tulishtaki individual (mtu binafsi).

Aliendelea kusisitiza: “Kimsingi, haihitaji hata kuweka dhamana ya chochote, haina umuhimu kwa sababu akishindwa si tunamkamata, tunamrudisha, tunaendelea na kesi mahakamani!”

Sethi na mfanyabiashara James Rugemalira walikamatwa na kushtakiwa Juni 2017 kwa uhujumu uchumi kutokana na tuhuma za uchotaji fedha katika Akaunti Maalumu ya Tegeta Escrow.

Walikabiliwia na mashtaka ya kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababishia Serikali hasara ya Dola za Marekani 22.1 milioni na Sh309.4 bilioni.

Baada ya kesi hiyo kukaa mahakamani kwa zaidi ya miaka minne, Sethi aliomba kufanya majadiliano ya DPP, ili kumaliza kesi hiyo chini ya utaratibu wa makubaliano ya kukiri kosa na Septemba 16 Rugemalira aliachiwa huru baada ya DPP kumfutia mashtaka.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyosikiliza kesi hiyo ilimtia Sethi hatiani na kumwamuru kulipa kiasi fidia kulingana na makubaliano na DPP na kumwachia huru.

Moja ya vipengele vya makubaliano hayo na DPP ni kwamba Serikali itakuwa huru kutaifisha mitambo hiyo na kiwanja, endapo atashindwa kulipa fidia kadiri ya makubaliano.

Maswali kuhusu dhamana

Wiki chache baada ya Sethi kuachiwa, Mahakama ya Rufani ilitoa uamuzi uliobatilisha uhamishiaji wa kampuni ya IPTL na mali zake, ikiwemo mitambo ya kufua umeme kwa PAP.

Miongoni mwa maswali yaliyoibuka ni nini hatima ya dhamana ya Seth aliyetumia mitambo ya IPTL kama dhamana? Je, hivi sasa mitambo hiyo inamilikiwa na nani?

Panda shuka ya IPTL

Licha ya masuala mengi ya kihistoria, Septemba 5, 2013, Jaji John Utamwa wa Mahakama Kuu alitoa uamuzi wa kuikabidhi IPTL na mali zake, ukiwemo mtambo wa kufua umeme, kwa PAP, kufuatia maombi yaliyofunguliwa na Rugemelira kupitia kampuni yake ya VIP Engineering and Marketing Limited.

Katika maombi hayo, VIP ambayo ilikuwa mbia mwenza katika IPTL ikimiliki asilimia 30 ya hisa, ilikuwa ikiondoa maombi yake ya ufilisi wa IPTL.

Iliomba pia mahakama hiyo iamuru hisa zake ndani ya IPTL zihamishiwe kwenye kampuni ya PAP (mali ya Sethi), kutokana na makubaliano ya mauzo ya hisa hizo.

Pia PAP iliwasilisha mahakamani taarifa kuwa ilikuwa tayari imeshanunua hisa 7 za kampuni ya Mechmar Corporation (Malaysia) Berhad (katika ufilisi), ambayo ilikuwa mwanahisa mkuu wa IPTL.

Mahakama Kuu ilikubaliana na maombi hayo na kuamuru masuala yote ya IPTL yawekwe chini ya PAP na ilitoa amri nyinginezo zikiwemo hisa za VIP kuhamishiwa kwa kampuni ya PAP na masuala yote ya IPTL kuwa chini ya PAP.

PAP iliahidi kulipa madeni yote ya IPTL, ambayo yangethibitika.

Mechmar haikuridhika na uamuzi huo na mwaka huohuo ilipeleka maombi ya mapitio Mahakama ya Rufani ikiiomba ipitie uamuzi wa Mahakama Kuu na kujiridhisha na uhalali wake.

Wadaiwa wengine walikuwa ni IPTL yenyewe, Kabidhi Wasihi Mkuu, ambaye alikuwa ameteuliwa kuwa mfilisi wa IPTL na PAP.

Wakati maombi hayo ya mapitio ya Mechmar yakiwa bado hayajasikilizwa na kutolewa uamuzi, PAP, kwa kutumia uamuzi wa Mahakama Kuu, ilimiliki na mali zote za IPTL ikiwemo Akaunti Maalumu ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa kwa pamoja kati ya Serikali kupitia Shirika la Umeme (Tanesco) na IPTL.

Akaunti hiyo ilifunguliwa kwa ajili ya kuweka fedha za malipo ya uwekezaji ambazo Tanesco ilipaswa kuzilipa kwa IPTL wakati ikisubiri kumalizika kwa mgogoro mahakamani na kujua kiwango sahihi ambacho Tanesco ilipaswa kukilipa.

Baada ya kumilikishwa IPTL, PAP ilichota fedha hizo.

Sehemu ya fedha hizo zilichukuliwa na Rugemalira kama malipo ya hisa zake alizokuwa akizimiliki IPTL.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live