Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DPP aridhia watuhumiwa mauaji kada CCM washitakiwe

74861a34ff69732e756f1c65da44a242 DPP aridhia watuhumiwa mauaji kada CCM washitakiwe

Thu, 1 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKURUGENZI wa Mashitaka nchini, Biswalo Mganga ameidhinisha watuhumiwa wanne waliokamatwa kwa tuhuma za mauaji ya Emmanuel Mlelwa mkoani Njombe, kufunguliwa mashitaka ya mauaji ya kukusudia.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa jana jijini Dodoma, Mganga alisema Ofisi ya Taifa ya Mashitaka imeridhia watuhumiwa hao wanne ambao Thadei Mwanyika,George Sanga, Optatus Nkwera na Goodluck Mfuse wafunguliwe mashitaka ya mauaji ya kukusudia, baada ya wao kukiri kumuua Mlelwa kwa kumnyonga hadi kufa.

Awali juzi, Polisi mkoani Njombe iliwashikilia watuhumiwa hao wanne kwa tuhuma za mauaji ya Mlelwa, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Vyuo Vikuu mkoani Iringa.

Katika taarifa hiyo, Mganga alisema Septemba 21, mwaka huu saa tisa na nusu jioni, mwili wa Mlelwa ulikutwa eneo la Bwawa la Kibena Estate kwenye daraja la Mtege mkoani Njombe.

Alisema taarifa za tukio hilo zilifikishwa Polisi ambao walichukua mwili na kuuhifadhi, kisha uchunguzi kuanza.

Alisema daktari aliyefanya uchunguzi mwili huo, alibainisha chanzo cha kifo cha Mlelwa ni ukosefu wa hewa na ndipo msako wa kuwasaka watuhumiwa ulianza na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wanne.

DPP alisema baada ya polisi kufanya upelelezi huo na kukamilika, jalada lilipelekwa ofisini kwake kufanyiwa uamuzi na alibaini mtuhumiwa Mwanyika ambaye ni mgombea udiwani mwaka huu katika Kata ya Utalingolo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alikiri kumuita marehemu usiku saa tano na kumteka.

“Mwanyika alieleza kuwa Septemba 20 usiku saa tano alimuita Mlelwa (marehemu sasa) kwenye baa iitwayo Tale iliyoko Njombe na kisha kumteka, na akawataja wenzake walioshirikiana naye kumteka kuwa ni Sanga ambaye ni Katibu wa Chadema Jimbo la Njombe Mjini na Nkwera ambaye ni Katibu Mwenezi wa Chadema Kata ya Ramadhani na Mfuse ni mkazi wa Njombe Mjini,” alisema DPP Mganga.

Alisema watuhumiwa wote walidai kuwa baada ya kumteka, walimuingiza kwenye gari aina ya Gaia yenye rangi ya fedha namba T 457 DAB na kumpeleka eneo la bwawa hilo, kisha wakamtesa na kumnyonga na kumtupa ndani ya bwawa.

Alisema mtuhumiwa Sanga alipopekuliwa nyumbani kwake, alikutwa na fulana mbili za Chadema moja ikiwa na matone ya damu na pia gari hiyo ilikutwa na ndani yake kulikuwa na mkanda wa suruali ya marehemu, ambao walidai waliutumia kumnyonga Mlelwa hadi kufa.

‘Nimepitia kwa makini ushahidi niliourejea kwa ufupi hapo juu na kujiridhisha kuwa unatosha kufungua mashitaka dhidi yao, hivyo kwa kuzingatia misingi ya Ibara ya 59B(4)(a) hadi (c) ya Katiba pamoja na masharti ya Sheria ya Usimamizi wa Mashtaka Namba 28 ya mwaka 2008, leo Septemba 30, mwaka 2020 nimeidhinisha mashtaka ya mauaji ya kukusudia kwa watuhumiwa hao wanne tajwa,” alisema Mganga.

Aidha, alitoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi kuendelea kufanya upepelezi ili kuwakamata watuhumiwa wengine, ambao bado hawajakamatwa na walihusika na tukio hilo.

Alitoa mwito kwa wananchi kuishi kwa amani,utulivu na mshikamano na kufuata sheria za nchi.

“Niwakumbushe wananchi kutunza usalama wa taifa letu ni jukumu la kila mmoja wetu, hivyo sote tunatakiwa kufichua na kutoa taarifa juu ya vitendo vyenye mwelekeo wa kuvuruga amani na usalama wa nchi yetu,” alisisitiza

Chanzo: habarileo.co.tz