Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DPP aomba mahakama imvumilie jalada kesi ya mke wa Bilionea Msuya

9557 Kesi+pic TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) ameiomba Mahakamani ya Hakimu Mkazi Kisutu, imvumilie wakati analifanyia kazi jalada la kesi ya mauaji inayomkabili mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita.

Hayo yameelezwa leo Agosti Mosi na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, wakati shauri hili lilipofikishwa kwa ajili ya kutajwa.

Mwita amedai kuwa baada ya kupewa maelekezo na mahakama ya kulifuatilia jalada hilo kujua limefikia hatua hiyo, alifanya hivyo na kulikuta jalada hilo likiwa bado lipo mikononi mwa DPP analifanyia kazi kwa sababu lina mambo mengi.

“DPP amekiri kupokea malalamiko kutoka kwa washtakiwa na wahanga wa tukio, hivyo bado analifanyia kazi kwa sababu jalada hili lina mambo Mengi" amedai Mwita na kuongeza;

“Kutokana na hali hiyo, DPP ameiomba mahakama yako, imvumilie wakati analifanyia kazi jalada hili, ili maamuzi atakayoyatoa yawe ya haki kwa pande zote," amedai Mwita.

Baada ya Maelezo hayo, Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala alidai kuwa kutokana na jalada hilo kufanyiwa kazi na DPP, mahakama itoe ahirisho ili DPP aweze kufanya kazi yake.

“Kwa kuwa tumepewa Maelezo na upande wa mashtaka kuwa DPP analifanyia kazi jalada hili na baadae atatoa maamuzi, ni rai yetu mahakama itoe ahirisho ili tumpe nafasi DPP aweze kufanya kazi yake" amedai Kibatala.

Soma Zaidi:

Jalada la kesi ya mke wa bilionea Msuya lipo kwa DPP

Hakimu Simba baada ya kusikiliza hoja za pande zote, aliutaka upande wa mashtaka kuhakikisha kuwa wanaendelea kufuatilia ili kujua DPP anamaliza lini kulifanyia kazi na kutoa maamuzi.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 14, mwaka huu itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz