Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DPP akabidhi mali za Sh4.4 bilioni zilizotaifishwa na Serikali

DPP DPP akabidhi mali za Sh4.4 bilioni zilizotaifishwa na Serikali

Tue, 4 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) imekabidhi Wizara ya Fedha na Mipango mali 8,188 zenye thamani ya Sh4.4 bilioni zilizotokana au zilizotumika kutenda uhalifu nchini.

Mali hizo zilikabidhiwa jana Jumatatu Oktoba 3, 2022 na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) Sylvester Mwakitalu kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba.

Mali hizo zimekusanywa katika mikoa mbalimbali ikiwemo Njombe, Morogoro, Dodoma, Kagera na Dar es Salaam.

Akizungumza Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, Chotto Sendo amesema makabidhiano hayo yanahusu nyumba 19, viwanja (9), mashamba mawili (2), vyombo vya moto (63), magari 31 na pikipiki (9).

Nyingine ni mbao (4,796), madumu (109) ya lita 20 kila moja ya mafutaa ya ndege/taa, mashine moja ya kukobolea mpunga na madini bati yenye uzito wa kilo 2,104.

“Katika kuhakiki tumekutana na changamoto mbalimbali kwamba kuna mali ambazo zina zaidi ya miaka mitatu, zimeanza kuharibika lakini vilevile wamiliki wa hizo mali wameendelea kuzitumia,” amesema.

Advertisement Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) Sylvester Mwakitalu amesema awali baadhi ya mali walizokabidhi Serikalini siku za nyuma, zilileta changamoto kwa washtakiwa kukataa rufaa na mahakama kutengua maamuzi ya mwanzo.

Amesema hiyo ndio sababu kuu ya mali hizo kuendelea kushikiliwa na ofisi yake kwa kipindi hicho ili kutoa nafasi kwa washtakiwa kutafuta haki zao zote kabla ya kuzikabidhi kwa Serikali.

Amesema kuwa mali wanazokabidhi leo hazina kipangizi kwasababu washtakiwa walipata nafasi ya kutafuta haki zao hadi mahakama za juu ama wengine waliridhika na uamuzi wa mahakama.

 “Kwa mujibu wa sheria zetu mhalifu hatakiwi kunufaika na mali alizopata kutokana na uhalifu. Kwasababu zikibaki kwa wahalifu zitatumika kufadhili uhalifu mwingine au zitawanufaisha wahalifu na kuonyesha jamii uhalifu unalipa,” alisema.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba amesema baada ya kukabidhiwa kwa mali hizo watafanya uchambuzi kuona zinazofaa kwa ajili ya matumizi ya Serikali ambazo watazigawa kwa taasisi za umma zikaendelee kutoa huduma na zisizofaa kwa matumizi ya Serikali zitapigwa mnada.

“Natambua ofisi yako iliwasilisha maombi ya mbao, sasa baadhi ya halmashauri ziliashatumia zilizokuwa zimehifadhiwa. Natoa rai kwa halmashauri hizo kwamba hiyo ni kinyume cha taratibu lakini tutawataka nao wawasilishe maombi tuweze kuyachambua,”amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live