Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DPP aagiza uchunguzi jinai ulanguzi saruji

0813dc77e340dcefab6b3cacf61ecd96 DPP aagiza uchunguzi jinai ulanguzi saruji

Sat, 21 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKURUGENZI wa Mashitaka, Biswalo Mganga ametoa siku 30 kuanzia jana ufanyike uchunguzi wa jinai juu ya tuhuma za uhaba wa saruji na vifaa vya ujenzi uliosababisha ongezeko la bei.

Amemwagiza Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI), Diwani Athumani pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), John Mbungo kufanya hivyo kwa mujibu wa kifungu cha 9(1)c na 17(1)na (2) cha sheria ya usimamizi wa mashtaka sura 30 marejeo 2019.

Alisema mara baada ya kupokea jalada husika la uchunguzi, atachukua hatua stahiki za kisheria kwa kuzingatia misingi inayomwongoza kama ilivyoainishwa katika ibara ya 59B ya katiba ya nchi na sheria nyingine za nchi.

Katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana, Mganga alisema kwa kipindi cha takribani mwezi mmoja sasa, amebaini uwapo wa tatizo la kupanda kwa bei ya saruji na vifaa hivyo vya ujenzi katika mikoa mbalimbali nchini.

"Mazingira ya suala hili, yanaashiria utendekaji wa makosa ya jinai katika mnyororo wa uzalishaji , usafirishaji na uuzaji wa bidhaa tajwa kwa wateja na hivyo kusababisha bidhaa hizo kuuzwa na kununuliwa kwa bei ya juu au kutopatikana kabisa kwenye maeneo mbalimbali nchini," alisema.

Alisema, “ ikumbukwe kuwa ni kosa la uhujumu uchumi kwa mujibu wa sheria ya uhujumu uchumi na uhalifu wa kupangwa kwa mtu yeyote mwenye leseni au asiye na leseni ya kufanya biashara.”

Vile vile kukutwa na bidhaa katika mazingira yanayoashiria kuunyima umma fursa ya kuinunua bidhaa husika kwa bei stahiki kunahesabiwa kuwa uhujumu uchumi.

Vitendo vingine vinavyotajwa kuwa chini ya kosa hilo ni kuuza bidhaa kwa bei juu au kwa masharti yaliyo kinyume na sheria pamoja na wakati wa kufanya biashara husika na kutengeneza makusudi mazingira yanayoweza kusababisha uhaba wa bidhaa katika soko.

Pamoja na ongezeko kubwa au kupungua kwa bei katika soko kinyume na sheria pia athari katika mgawanyiko sawa na usambazaji wa bidhaa katika soko kwa wanunuzi katika eneo husika.

"Vitendo tajwa hapo juu ni makosa kinyume na sheria tajwa hapo na endapo wahusika watafikishwa mahakamani na kutiwa hatiani, wanaweza kuhukumiwa kifungo cha kati ya miaka 20 hadi 30 gerezani," alisema.

Alisema mali na bidhaa zitakazohusika katika uhalifu huo zinaweza kutaifishwa na mahakama na kuwa mali ya serikali kwa mujibu wa sheria.

Chanzo: habarileo.co.tz