Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DPP Tanzania atoa onyo kwa wanaojihusisha na uhalifu

Thu, 4 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya vigogo wa kampuni ya mawasiliano ya simu za mkononi ya Vodacom kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP) Biswalo Mganga, amesema ofisi yake haitamuonea haya mtu yeyote atakayejihusisha na uhalifu hata kama ana wadhifa mkubwa.

Mganga amesema hayo jana Jumatano Aprili 3, 2019 muda mchache baada ya mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Vodacom Tanzania, Hisham Hendi na wenzake wanane kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 20/2019 iliyopo mahakamani hapo.

Hendi na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 10, likiwamo la kuongoza genge la uhalifu na kuisababishia hasara Serikali ya Sh5,892,513,000.

Mganga amesema wakurugenzi hao wa Vodacom wameunganishwa katika kesi hiyo kwa sababu ndio wameongoza genge la uhalifu kwa kusaidia kuingizwa kwa mitambo ambayo haikupata kibali na kusababisha hasara.

Mganga amesema kampuni hiyo ya Tala, ofisi zake zipo nchini Kenya na kwamba wakurugenzi wake wapo nchini Marekani hivyo imesababisha hasara kwa Serikali kwa kuendesha shughuli zao na kuingiza mitambo bila leseni.

‘’Niseme tu hapa hakuna siasa katika suala hili, najua mengi yataongelewa lakini tunapaswa kutambua uhalifu ni uhalifu hatutajali ni nani aliyefanya hivyo wala ana fedha kiasi gani au ana wadhifa gani atafikishwa tu mahakamani,” amesema Mganga na kuongeza:

“Natoa onyo kwa kampuni nyingine ambazo zinafanya hivyo, kwa sasa tunaendelea na uchunguzi na kitakachobainika kitawekwa wazi.”

Naye mwanasheria wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Johannes Kalungula amesema kampuni ya Vodacom imefanya ulaghai kwenye mawasiliano kwa kugawa namba au masafa ambayo TCRA pekee wenye mamlaka ya kufanya hivyo.

“TCRA ndio tuna wajibu wa kutoa namba au masafa, sasa tunashangaa kampuni ya Vodacom wao walikuwa wanagawa masafa,” amesema Kalungula.

Kalungula amesema kampuni inayocheza na masafa hayo, mitambo yao iko imara na inawamulika hivyo watawachukulia hatua na kwamba licha ya kukaribisha wawekezaji, wanapaswa kufuata taratibu za nchi.

Mbali na Hisham, washtakiwa wengine ni mkuu wa kitengo cha mapato wa Vodacom PLC, Joseph Nderitu ambaye ni raia wa Kenya, mkurugenzi wa sheria wa kampuni hiyo, Olaf Mumburi mkazi wa Victoria Kinondoni.

Wengine ni mkuu wa kitengo cha mauzo wa kampuni hiyo, Joseph Muhere; meneja  fedha, Ibrahim Bonzo na kampuni ya Vodacom Tanzania iliyopo Ursino Estate barabara ya Bagamoyo.

Washtakiwa wengine ni Brian Lusiola, mtaalamu wa teknolojia ya habari ambaye ni raia wa Kenya;  meneja uendeshaji biashara wa kampuni ya Inventure Mobile Tanzania Ltd, Ahmed Ngassa na kampuni ya Inventure Mobile Tanzania Limited T/A Tala Tanzania.

Akisoma mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, wakili wa Serikali, Jacqueline Nyantori akisaidiana na Wankyo Simon, alidai katika mashtaka ya kwanza, mshtakiwa Hendi, Nderitu, Mumburi, Muhere na Bonzo, wanadaiwa  kati ya Januari mosi 2018 na Machi 11, 2019 maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, kinyume na sheria waliongoza genge la uhalifu na kuisababishia Serikali hasara ya Sh5.8 bilioni kupitia TCRA.

Katika shtaka la pili,  Ngassa, Lusiola na Kampuni ya Inventure Mobile Tanzania Ltd/ A Tala Tanzania, wanadaiwa kuingiza vifaa vya kieletroniki bila kuwa na leseni ya TCRA huku wakijua kuwa ni kinyume cha sheria.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote mahakamani hapo kutokana na kesi inayowakabili kutokuwa na dhamana.

Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 17, 2019 itakapotajwa na washtakiwa walirudishwa rumande.

 

 



Chanzo: mwananchi.co.tz