Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DED mbaroni kwa upotevu wa fedha

15266 Pic+ded TanzaniaWeb

Mon, 3 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nyang’wale. Vigogo wawili wa halmashauri ya Nyang’wale, mkoani Geita wamekamatwa kwa tuhuma za upotevu wa Sh2 bilioni za miradi ya maendeleo.

Waliokamatwa ni aliyekuwa mkurugenzi mtendaji (DED) wa Halmashauri ya Nyang’wale, Carlos Gwamagobe na mweka hazina, Donatus Pangani.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel alisema jana kuwa mbali ya viongozi hao, watumishi wengine wanane wakiwamo wakuu wa idara wanahojiwa na katibu tawala wa mkoa amekwenda wilayani humo na timu yake kuanza ukaguzi.

Sakata la fedha hizo lilibainika wakati wa makabidhiano ya ofisi Agosti 30, baina ya mkurugenzi aliyemaliza muda wake na mkurugenzi mpya baada ya fedha zilizopo kwenye akaunti ya halmashauri kutofautina na taarifa ya makabidhiano.

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’wale Hamimu Gwiyama aliyeshuhudia makabidhiano hayo alisema baada ya kutilia shaka suala hilo, walimtaka aliyemaliza muda wake atoe maelezo ya zilipo fedha za miradi.

Alisema uchunguzi wa haraka uliofanywa umebaini Sh2 bilioni hazijulikani zilipo.

Gwiyama alisema Serikali imeshatoa Sh1.6 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la halmashauri na kwa maelezo yaliyopo, Sh650 milioni zimeshatumika na kilichobaki ni zaidi ya Sh900 milioni lakini kwenye makabidhiano hazionekani kwenye akaunti ya halmashauri.

Alisema pia Sh719 milioni zilizotolewa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu ya shule za msingi na sekondari zaidi ya Sh500 milioni pia hazionekani kwenye akaunti. Alisema katika miradi ya afya, Serikali ilitoa Sh400 milioni kwa ajili ya uboreshaji wa Kituo cha Afya cha Nyang’wale na katika makabidhiano fedha zilizopo kwenye akaunti ni Sh10 milioni wakati mradi wenyewe haujaanza.

Alisema alipomuuliza mtuhumiwa alidai kuwa fedha hizo alizitumia kwa shughuli za halmashauri ikiwamo utengenezaji wa madawati, “Lakini hakuna taarifa inayoonyesha utaratibu uliotumika kubadili matumizi ya fedha hizo.”

Chanzo: mwananchi.co.tz