Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DDP aipa mamlaka, Mahakama ya Kisutu kusikiliza kesi ya 'ustadhi' wa meno ya tembo

54684 DPP+pic

Tue, 30 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.  Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), ameipa Mamlaka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili, Mohamed Mboweto (42) maarufu kwa jina la Ustadhi na wenzake saba.

Mboweto ambaye ni mkazi wa Mbagala Kiburugwa na wenzake, wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwemo la kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh 1.466bilioni.

DPP amewasilisha hati ya kuipa mamlaka, mahakama hiyo, leo Aprili 29, 2019 kupitia kwa wakili wa Serikali, Candidi Nasua, wakati kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.

Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa shauri hilo kukamilika.

Kwa kawaida kesi za uhujumu uchumi huwa zinasikilizwa Mahakama Kuu, Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi, lakini DPP akiona inafaa kulingana na mazingira anaweza kutoa hati ya kuipa Mamlaka, Mahakama ya chini kusikiliza kesi hizo.

Baada ya kuwasilisha hati hiyo ya kuruhusu kesi hiyo kusikilizwa mahakamani hapo, washtakiwa hao kwa mara ya kwanza walisomewa mashtaka yao  yanayowakabili.

Hata hivyo, washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao , walikana kutenda makosa hayo.

Baada ya washtakiwa kusomewa mashtaka yao, Hakimu Mkazi Mkuu, anayesikiliza shauri hilo, Huruma Shaidi, alisema kuwa mahakama imepokea hati mbili zilizowasilishwa na DPP, hivyo kesi hiyo itasikilizwa katika Mahakama ya Kisutu.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu  Shaidi, amepanga Mei 13, 2019, upande wa mashtaka kuwasomea washtakiwa hao  hoja za awali(PH).

Awali, wakili wa Serikali  Candidi Nasua, amedai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba DPP amewasilisha nyaraka za kuruhusu mahakama ya Kisutu kusikiliza kesi hiyo.

“Kwa ridhaa ya mahakama yako, tunaomba kuwasilisha hati ya kuruhusu mahakama ya Kisutu kusikiliza shauri hili la uhujumu uchumi, iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Biswalo Mganga” amedai Nasua.

“Pia tunaomba kuwasilisha hati ya kuipa Mamlaka, Mahakama ya Kisutu, kuendesha kesi hii ya uhujumu uchumi” amedai Nasua.

Mbali na Mboweto, washtakiwa wengine katika hiyo ya uhujumu uchumi namba 4/2016 ni Robert  Mwaipyana (32) mkazi wa Mabibo; Ramadhani Mnekea(55) dereva na mkazi wa Temeke; Ramadhan Matimbwa(42).

Wengine ni Exavery Silvester(36) dereva na mkazi wa Masasi mkoani Mtwara; Frank Sadik (51) mkazi wa Mtwara; Issa Pilla(43) mfanyabiashara na mkazi wa Masasi na Cliford  Maivaji(51) mfanyabiashara na mkazi wa Temeke.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwemo la  kujihusisha na mtandao wa ujangili.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kati ya Januari mosi, 2015 na Desemba 21, 2015, katika maeneo ya Dar es Salaam na Mtwara, walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza  vipande 161 vya meno ya tembo.

Nasua alidai vipande hivyo vina  uzito wa kg 220.96 na vina  thamani ya dola za Marekani 690,000, ambazo ni sawa na Sh 1,466,250,000, mali ya Serikali ya Tanzania na kwamba washtakiwa hao walikuta na nyara hizo, bila kuwa na kibali  cha Mkurugenzi wa Wanyama Pori nchini.

Washtakiwa wamerudishwa  rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.



Chanzo: mwananchi.co.tz