Matukio ya kupotea, kushambuliwa, kuteswa na kuuawa kwa baadhi ya watu wakiwemo wanahabari, wanasiasa na wasanii, sasa yamekabidhiwa mahakamani baada ya mamlaka zenye dhamana ya upelelezi kushindwa kutoa taarifa za upelelezi wa matukio hayo.
Matukio hayo yamefikishwa mahakamani na mwanahabari na mwanaharakati wa haki za binadamu, Luqman Maloto aliyefungua shauri la maombi ya jinai Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam dhidi Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).
Katika shauri hilo namba 5 la mwaka 2023, Maloto pamoja na mambo mengine anaiomba mahakama hiyo itamke DCI anawajibika kwa maisha ya watu aliowataja ambao wamo waliopotea, walioshambuliwa na kuteswa na waliouawa kwa kuwa wajibu wake ni kulinda maisha ya Watanzania.
Maloto amewataja waathirika hao ni pamoja mwanahabari Azory Gwanda na wanasiasa Ben Saanane, Simon Kanguye, Daniel John, Tundu Lissu, Mdude Mpaluka Nyagali maarufu kama Mdude, Leopord Lwajabe, Akwilina Akwilini, Ibrahim Mshana maarufu kama Roma Mkatoliki na Allan Kiluvya.
Pia anaiomba mahakama hiyo itamke DCI ameshindwa ama kwa kutokuwa na uwezo au kwa makusudi kufanya upelelezi kuhusu madhila yaliyowakuta watu hao kutokana na kushindwa kutoa taarifa kwa umma na kwa familia za waathirika hao kuhusu madhila yaliyowapata.
Hivyo, anaiomba mahakama hiyo itamke kwamba kuchelewa au kushindwa kukamilishwa kwa upelelezi dhidi yao hakuongozwi na kanuni yoyote na itoe amri dhidi ya DCI kuwasilisha mahakamani hapo taarifa yenye maelezo ya kina kuhusu kupotea, kuuawa na kuteswa kwao, kwa uchunguzi zaidi. Shauri limepangwa kusikilizwa na Jaji John Nkwabi na litatajwa Februari 8 mwaka huu.
Azory Gwanda
Gwanda alikuwa mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi, akiripoti kutokea Kibiti Mkoa wa Pwani.
Alijikita zaidi kuripoti taarifa za ukiukwaji wa haki na usalama kutokana na wimbi la mauaji yaliyotikisa wilayani Kibiti yaliyowalenga kwa kiasi kikubwa maofisa wa Serikali za mitaa na maofisa wa Polisi, mwaka 2016 na 2017, alipotea katika mazingira ya kutatanisha Novemba 21, 2017.
Kwa mujibu wa mke wa Gwanda, Anna Pinoni, siku hiyo mumewe alifika shambani alikokuwa akilima akiwa na watu wanne katika gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe, alimuita akamuuliza mahali uliko ufunguo wa nyumbani.
Baada ya mkewe kumwelekeza alikoweka ufunguo, alimuaga kuwa anakwenda kazini na amepata safari ya dharura, hivyo kama asingerudi siku hiyo, angerudi kesho yake.
Baada ya mkewe kurudi nyumbani alikuta nyumba imevurugwa, ikionyesha ilikuwa imepekuliwa.
Baada ya kupita siku mbili bila kurejea huku kukiwa hakuna mawasiliano kwenye simu zake, mkewe alitoa taarifa kituo cha Polisi Kibiti Novemba 23 na mpaka sasa hajajulikana mahali aliko kama yuko hai au alishafariki dunia na hakuna taarifa iliyowahi kutolewa na vyombo vya uchunguzi.
Tundu Lissu
Lissu ambaye sasa ni makamu mwenyekiti wa Chadema-Bara, alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 akiwa ndani ya gari lake, wakati huo akiwa mbunge wa Singida Mashariki.
Tukio hilo lilitokea baada ya kuwasili katika makazi yake Area D, jijini Dodoma mchana kweupe.
Siku hiyo hiyo usiku, Lissu alipelekwa Nairobi, nchini Kenya alikotibiwa hadi Januari 6, 2018, alipohamishiwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi ambako anaishi mpaka sasa.
Tayari ameshatangaza kurejea nchini Januari 25 mwaka huu kushiriki harakati za kisiasa na chama chake.
Jeshi la Polisi limekuwa likieleza limeshindwa kukamilisha upelelezi wake, kwani linamsubiri aje nchini kwa ajili ya kuhojiwa.
Ben Saanane
Bernard Saanane maarufu Ben Saanane alikuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Novemba 14, 2017 ilikuwa siku ya mwisho kuonekana ofisi za makao makuu ya chama hicho zilizopo Mtaa wa Ufipa, Kinondoni, Dar es Salaam, kwani aliwaaga wenzake alikuwa anajiandaa kwenda Afrika Kusini.
Aliondoka nyumbani kwake Mabibo Novemba 15, 2017 na hakurejea na mpaka sasa haijulikani alipo.
Taarifa kupitia mawasiliano yake zilionyesha siku hiyo alitumia saa kadhaa eneo la Mikocheni baadaye jioni simu yake ilitumika kutoa Sh50,000 kwa wakala wa M-Pesa aliye eneo la Mburahati na baada ya hapo utambuzi wa simu yake ukapotea.
Taarifa za kupotea kwake ziliripotiwa kituo cha polisi Tabata, Dar es Salaam, lakini mpaka sasa Jeshi la Polisi halijawahi kutoa taarifa za upelelezi juu yake.
Simon Kanguye
Alikuwa diwani wa Kibondo, kada wa CCM na mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo na alitoweka Julai 20, 2017 baada ya kuchukuliwa ofisini kwake na watu wasiojulikana na hadi leo haijulikani alipo.
Mkewe Mariamu Gwiboha aliwahi kusema kabla ya tukio hilo aliwahi kumwambia kuhusu azma ya kuwasilisha malalamiko kwa Rais John Magufuli kuhusu watu waliokuwa wanaeneza uvumi kwamba hatakiwi kuwa mwenyekiti wa halmashauri hiyo.
Akwilina Akwilini
Alikuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Mabibo jijini Dar es Salaam.
Alifariki dunia Februari 16, 2018 kwa kupigwa na kitu kilichosadikiwa kuwa risasi akiwa kwenye daladala baada ya vurugu kuibuka wakati maofisa wa polisi wakizuia maandamano ya viongozi, wanachama na wafuasi wa Chadema.
Wafuasi hao walikuwa wakiandamana kuelekea ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kudai barua za mawakala wao, baada ya kufunga mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni, uliofanyika Oktoba 18, 2018.
Daniel John
Alikuwa Katibu wa Chadema, Kata ya Hananasif, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam na alipotea Februari 12, 2018 na baadaye mwili wake ulipatikana katika ufukweni jijini Dar es Salaam (Coco Beach).
Mdude Nyagali
Mei 4, 2019 Mdude aliyekuwa kiongozi wa mafunzo Kanda ya Nyasa Chadema, aliripotiwa kutekwa na watu wasiojulikana na aliokotwa na madereva bodaboda katika kitongoji cha Mtakuja, Kijiji cha Inyala wilayani Mbeya Mei 8, akiwa hoi kutokana na kipigo alichokipata.
Leopold Lwajabe
Alikuwa Ofisa Mwandamizi Wizara ya Fedha na Mipango, mkurugenzi wa miradi inayotekelezwa na Umoja wa Ulaya nchini (EU) kupitia wizara hiyo.
Lwajabe alifariki katika mazingira tata, kwani mwili wake ulikutwa wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani ukining’inia juu ya mti wa mwembe Julai 26, 2019.
Roma Mkatoliki
Ibrahim Mussa ‘Roma Mkatoliki’ ambaye ni msanii wa muziki wa Hip hop, Aprili 7, 2017 akiwa na wenzake watatu walichukuliwa na watu wasiojulikana wakiwa kwenye Studio ya Tongwe Records iliyopo Masaki, Dar es Salaam wakifanya kazi ya kurekodi nyimbo.
Walikaa mikononi mwa watu hao hadi Aprili 9, walipoachiwa. Baadaye wakizunguma na vyombo vya habari, Roma alisimulia kuwa watu hao walipowateka waliwapeleka kwenye gari, wakawafunga macho kwa vitambaa na kuanza kuwahoji, huku wakiwatesa, lakini hajawahi kusema walichokuwa wakiwahoji.
Allan Kiluvya
Alikuwa msaidizi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe. Julai 6, 2019 aliripotiwa kupotea baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana usiku na alipatikana Julai 8.
Alinukuliwa na vyombo vya habari akieleza kuwa watekaji walimpeleka hadi eneo la njiapanda ya Segerea baada ya kumuuliza ni mahali gani ingeweza kuwa rahisi kufika nyumbani kwake.