Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC aunda timu kusaka magenge ya wahalifu

F367c867f3492070227d0adbf1196e3c.png Wilson Shimo

Sun, 17 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ameunda kikosi kazi kwa ajili ya kuwasaka na kuwakamata vijana wanaojihusisha na magenge ya uhalifu.

Shimo amekiri kuchukua hatua hiyo kutokana na fununu za uwepo wa makundi ya vijana kwenye maeneo tofauti wanaodaiwa kutekeleza vitendo vya unyang’anyi, uporaji na ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.

Alibainisha hayo mwishoni mwa wiki wakati akifanya mahojiano na waandishi wa habari juu ya mikakati ya wilaya kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia na kingono kwa watoto wa mtaani.

“Niendelee kuwaomba wananchi wenzangu, kwa yeyote ambaye ana tabia na hulka mbaya ya kuwafanyia vitendo vya ukatili watoto hawa ambao wapo mtaani, kama vile ulawiti, tumeshaanza kuchukua hatua,” alisema.

Alisema tayari wanamshikilia mtu mmoja kwa tuhuma za kulawiti watoto wa mtaani ambao wamekuwa wakilala katika kituo kikuu cha mabasi ya abiria mjini Geita na kwamba bado uchunguzi unaendelea.

Mlinzi wa kituo hicho cha mabasi, Tazani Amri aliwaambia waandishi wa habari kwamba amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa watoto wa mtaani wakidai kuna mtu amekuwa akiwafuata nyakati za usiku kwa lengo la kuwafanyia vitendo viovu.

Tazani alisema baada ya kuongea na baadhi ya watoto hao alibaini miongoni mwao tayari wameshafanyiwa vitendo vichafu na mtu huyo anayetajwa kutumia nondo, msumari na wembe kuwatishia watoto hao.

“Nilisikia vijana walikuwa wanalia, sasa nilipotoka kwenye eneo langu kuja kupeleleza nikakuta vijana wanapigana, nikawa nimewahoji wakasema kwamba kuna kijana huwa anakuja usiku kuwafanyia mchezo mchafu,” alieleza.

Mmoja ya watoto hao alikiri kufanyiwa kitendo kibaya akisema: “Akanipeleka kule, akaniambia kaa hapo. Alikuwa na msumari na jiwe. Akaniambia dogo unanijua mimi, akaanza kunivua nguo kwa lazima. Nikaanza kulia.”

Lakini mpiga debe wa kituo hicho cha mabasi, Frank Mgaya alisema kero ya watoto wa mtaani imeongezeka sana kituoni hapo, wengi akisema wanajishughulisha na kuokota chupa na kuuza.

Aliviomba vyombo vya usalama kuchukua hatua zaidi na kuzitaka familia kuwa makini ili zisizalishe watoto wa mitaani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live