Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DC ataka majina ya vijana waliotoweka miezi 6 sasa

Afc44c8d7721415159a4733077610b0d DC ataka majina ya vijana waliotoweka miezi 6 sasa

Sat, 9 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Wilaya ya Mtwara, Danstan Kyobya amemuagiza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Vijijini kumpa taarifa kuhusu uwepo wa watoto na vijana ambao hawafahamiki walipo kwa kipindi cha miezi sita.

Kyobya alitoa kutoa mwezi mmoja kwa watendaji wa halmashauri hiyo, kumpa taarifa kuhusu walipo watoto na vijana ambao hawaonekani wilayani hapa na waeleze wameenda wapi na wanafanya nini.

“Nataka kupata watoto na vijana wote ambao hawafahamiki walipo kwa kipindi cha miezi sita, nipate taarifa hiyo ndani ya mwezi mmoja, waeleze wako wapi, wameenda wapi na wanafanya nini,” alisema.

Alitoa agizo hilo wakati akizindua Soko la kisasa la Samaki la Kijiji cha Msangamkuu katika halmashauri hiyo.

Alimuagiza pia mwenyekiti wa halmashauri hiyo, kupitia baraza la madiwani na kamati za ulinzi, kujadili kwa kina na kuwatambua watu wote katika halmashauri hiyo ili kubaini nani ni nani kwa ajili ya usalama wa wananchi wilayani humo.

Kyobya alisema kuna baadhi ya vijana wanadanganywa na kwenda sehemu nyingine na kuacha shule. Alisema mwenyekiti na watendaji wengine katika halmasharui hiyo, wanapaswa kusimamia utoro shuleni kuhakikisha watoto wanabaki shuleni.

“Mwenyekiti kupitia baraza lako na kamati zako ninataka mjadili kwa kina na kuhakikisha tunajua nani ni nani katika vijiji vyetu katika maeneo yetu, wengine wanakuja hatuwafahamu lakini wanakuja kutuharibia maisha yetu,” alisema.

Alisisitiza wenyeviti wa vijiji na vitongoji na kata, kuwatafuta watoto watoro wa shule. Alimtaka ofisa elimu msingi na sekondari kusimamia suala hilo.

Kyobya liwataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote wanaenda shule ifikapo Januari 11, mwaka huu na waanze kufanya maandalizi kuanzia sasa.

“Kila mzazi ahakikishe mtoto anaenda shule, kama mtoto hataenda shule mzazi husika atawajibika, maandalizi ya kwenda shule yafanyike sasa hivi kwa sababu serikali inatoa elimu bure, kazi ya wazazi ni kuwanunulia watoto wao nguo za shule tu na kuwapeleka shule,”alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz