Wakala wa Mabasi Yaendayo Kasi (DART), umemtimua mzabuni aliyekuwa akifanya kazi za usafi, Kampuni ya MOMA Trading Company baada ya kukutwa na kosa la kuwasilisha risiti feki za kielekroniki (EFD) kwa wakala huyo.
Taarifa ya kutimuliwa kwa kampuni hiyo imetolewa jana na Mtendaji Mkuu wa DART, Dk. Edwin Mhede wakati wa mahojiano baina yake ya Tanzania PANORAMA Blog yaliyofanyika makao makuu ya DART, Ubungo Maziwa kuhusu skandali ya malipo yaliyofanywa na wakala huyo kwa watoa huduma waliowasilisha risiti feki za kielektroniki.
Skandali ya kuwepo risiti feki za kielektroniki zilizofanyiwa malipo na DART kwa baadhi ya watoa huduma wake iliibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2021/22 iliyobainisha kuwa wakala huyo alifanya malipo ya Shilingi milioni 135.82 kwa kutumia risiti feki za kielektroniki.
Akijibu kwa niaba ya Dk. Mhede, Mkurugenzi wa Fedha na Maendeleo ya Biashara wa DART, Deus Kazimili alisema baada ya kupokea ripoti ya CAG iliyokuwa ikionyesha kuwepo kwa skandali hiyo, ofisi yake ilifanya uchunguzi wa risiti za kielektroniki ilizopokea kutoka kwa watoa huduma na kubaini risiti zilizowasilishwa na Kampuni ya MOMA ndizo zilizokuwa na dosari.
Alisema wakati wa uchunguzi huo ilibainika nyaraka za kudai malipo za Kampuni ya MOMA zilikuwa na kasoro ya risiti moja ya kielektroniki kutumika kwenye nyaraka zaidi ya moja za kudai malipo.
Kazimili alisema ofisi yake ilifanyi ukaguzi kwenye msimbo poa (Barcode) ulioko kwenye kila risiti ya kielektroniki ambapo risiti nane zilibainika kuwa sahihi lakini zilijirudia kwenye kudai malipo na moja ilibainika ni ya kughushi kwani haikuwiana hata kidogo na mifumo ya Mamlaka ya Mapato (TRA).
Alisema baada ya kulibaini hilo, hatua ya kwanza iliyochukuliwa na DART ni kuitaka Kampuni ya MOMA kuwasilisha upya nyaraka zilizopelea kwenye madai yake na risiti iliyobainika kuwa ni feki iliiondolea sifa kampuni hiyo kuendelea kufanya kazi na wakala huyo.
Kazimili alisema DART ilichukua hatua kali ya kumfukuzilia mbali mzabuni huyo kwa kosa la kuwasilisha risiti feki ya kielektroni na kwamba hivi sasa imeanzisha utaratibu wa kukagua msimbo poa katika kila risiti ya kielektoniki inayoipokea kutoka kwa wauzaji ili kudhibiti udanganyifu kwenye malipo.
Katika ripoti yake, CAG ameeleza kuwa DART walifanya malipo ya jumla ya Shilingi milioni 135.82 kwa wauzaji mbalimbali ambapo walipatiwa risiti za kielektroniki lakini wakati wa uthibitisho wa uhalali wa risiti hizo kwenye mfumo wa TRA zilibainika kuwa ni risiti feki.
“Kanuni ya 48 ya kanuni za usimamizi wa kodi za mwaka 2016, inasema mtu yeyote ambaye kwa makusudi anachezea au kusababisha kifaa cha kielektroniki kufanya kazi vibaya atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani atatozwa faini au kifungo au vyote kwa pamoja.
“Kuambatanisha risiti za EFD za kughushi kunamaanisha kuwa taarifa za mauzo kwenye miamala iliyothibitishwa na risiti za kughushi za EFD hazikufika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa hiyo kodi stahiki haiwezi kukusanywa na Serikali,” anasema CGA katika ripoti yake.
CAG anapendekeza kuwa Menejimenti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahusika walioghushi risiti za kielektroniki kwenye malipo yaliyofanywa na DART.