Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chonji akiri kukutwa na dawa za kulevya nyumbani kwake kwenye sufuria

Chonji Pic Chonji akiri kukutwa na dawa za kulevya nyumbani kwake kwenye sufuria

Fri, 11 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Maelezo ya onyo yanayodaiwa kuchukuliwa na polisi yameeleza namna mfanyabiashara Muharami Abdallah maarufu kama Chonji alivyokutwa na pakiti 24 za dawa za kulevya nyumbani kwake eneo la Magomeni Makanya zikiwa ndani ya kabati lake la nguo pamoja na kwenye sufuria.

Wakili Serikali, Titus Aron na Enock Kamala akiwasomea maelezo ya ushahidi na vielelezo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio alidai kuwa mashahidi wanaotegemea kutoa ushahidi 12, vielelezo vya maandishi saba na vielelezo 12.

Chonji na wenzake wanne inadaiwa

Oktoba 21, 2014 eneo la Magomeni Makanya Wilaya ya Kinondoni, walisafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 5309.57 na cocaine zenye uzito wa gramu 894.28.

Katika maelezo ya onyo mshtakiwa Chonji alikiri kukutwa na pakiti 24 za dawa za kulevya nyumbani kwake.

Maelezo hayo yanadai kuwa kabla ya mshtakiwa huyo kukamatwa alikuwa mfanyabiashara wa kuuza magari ambaye alikuwa anasafiri nchi mbalimbali ikiwemo Pakistan,Uholanzi na Dubai.

Katika maelezo hayo inadaiwa kuwa Oktoba 21, 2014 saa 6 usiku waliingia askari polisi wengi nyumbani kwake na kuanza kufanya upekuzi ndani ya nyumba yake na kukutwa pakiti 24 zinazodhaniwa dawa za kulevya lakini hakujua dawa hizo zilikuwa za nani.

Maelezo hayo yanadai kuwa wakati wanafanya upekuzi huo alikuwa na marafiki na wadogo zake ambao walikuwa wanamsaidia kuuza magari ambao ni Abdul Chumbi, Rehani Umande, Tanaka Mwakasagule na Maliki Maunda.

Katika maelezo ya SP Salmin yanaeleza kuwa Oktoba 21, 2014 saa 6 usiku walifanya upekuzi katika nyumba ya Chonji iliyopo Magomeni Makanya ambapo mshtakiwa huyo alifungua kabati na kutoa pakiti 15 za dawa za kulevya hizo alizoficha kwenye nguo.

Inadai kuwa baada ya kupata pakiti 15 za dawa hizo walielekea kwenye korido ya nyumba hiyo na kukutwa dawa za kulevya zikiwa ndani ya sufuria pakiti tisa na walipoenda kwenye chumba kingine walikuta fedha mbalimbali ikiwemo Dola za Marekani 24, Uro 50 na fedha taslimu kiasi cha Sh900,000.

Katika maelezo hayo yanadai pia walikuta kwenye chumba hicho mifuko ya plastiki meusi na meupe, soltepu ya kufungia dawa hizo, mizani mitatu ya kupimia dawa hizo.

Baada ya kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo hiyo Hakimu Mrio aliwauliza washtakiwa hao kama wana kitu cha kuongea walidai watakuwa na mashahidi pamoja na vielelezo wakati wakitoa utetezi wao.

Hakimu Mrio alisema kesi hiyo inahamishiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza kusikiliza mashahidi.

Mbali na Abdallah washtakiwa wengine katika shauri hilo ni Abdul Chumbi, Rehani Umande, Tanaka Mwakasagule na Maliki Maunda wote wakazi wa Magomeni Makanya.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Oktoba 21, 2014 katika eneo la Magomeni Makanya wilaya ya Kinondoni, walisafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 5,309.57.

Shtaka la pili, siku na eneo hilo, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina cocaine zenye uzito wa gramu 894.28.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live