Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CUF yawafikisha kortini waliochoma bendera, kubadilisha ofisi zake

48759 Cufpic

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) kimefungua kesi dhidi ya watu wote walioshiriki kuchoma bendera na kubadilisha rangi za ofisi zake visiwani Zanzibar na kuweka za chama cha ACT- Wazalendo.

Kesi hiyo namba 16 ya mwaka 2019 ilifunguliwa jana katika Mahakama ya Vuga iliyopo mjini Unguja, Zanzibar.

Akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa CUF, Khalifa Suleiman Khalifa amesema wamekusanya ushahidi wote wa vitendo vilivyofanywa na waliokuwa wanachama wachama hicho ambao wamemfuata aliyekuwa katibu mkuu kabla yake, Maalim Seif Sharif Hamad aliyehamia ACT-Wazalendo.

"Maalim Seif na viongozi wenzake wa CUF walitoa agizo kwamba bendera za CUF zishushwe. Kitendo cha kushusha bendera na kuzichoma ni uvamizi wa ofisi, ni jinai.”

“Sisi hatukutaka kupambana nao kwa kuwa hatuna nguvu, lakini tunajua sheria ndiyo maana tumelifikisha suala hili mahakamani," amesema Khalifa.

Katibu Mkuu huyo wa CUF amewataka Wazanzibar kufuata sheria na kuachana na vitendo vya kukihujumu chama hicho kwa kubadilisha ofisi zake kuwa za ACT-Wazalendo, vitendo ambavyo amesema ni jinai.

"Kwa kuwa mimi ndiyo katibu mkuu mpya, nitahakikisha kwa uwezo wa Mungu ninasimamia mali za CUF zinabaki kuwa mali za CUF.”

"Kuna usemi wao wanasema shusha tanga, pandisha tanga. Lakini wakumbuke wanaweza kuishia matanga," amesema kiongozi huyo ambaye amechukua nafasi ya Maalim Seif.

Kuhusu wabunge wa CUF ambao walikuwa upande wa Maalim Seif, Khalifa amewataka wafike ofisi za CUF kuonana na mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ameahidi kushirikiana nao katika kukijenga chama hicho na kusahau tofauti zao.

"Wabunge wale wajue kwamba waliingia bungeni kwa tiketi ya CUF, wasidhani waliingia kwa tiketi ya Maalim Seif. Yote yamepita, tunachotaka wafike ofisini kumuona mwenyekiti wetu. Hatutakuwa tayari kuona wanatumia rasilimali za chama kuimarisha ACT Wazalendo," amesema Khalifa.

Soma Zaidi>>>Waliochoma bendera, kuvamia ofisi za CUF wapelekwa mahakamani



Chanzo: mwananchi.co.tz