Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bwege, wenzake wakwama kortini

28437 Bwege+pic TanzaniaWeb

Fri, 23 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hitilafu kwenye barua za wadhamini zimesababisha viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) akiwamo mbunge wa Kilwa Kusini, Seleman Bungara maarufu kama Bwege kulazimika kulala mahabusu kwa siku ya nne.

Viongozi hao walifikishwa jana katika Mahakama ya Mkoa wa Lindi mbele ya hakimu Lilian Rugarabamu na kusomewa makosa yao na mwendesha mashtaka wa Serikali, Abdulrahman Mohamed.

Mohamed alidai kuwa washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kutishia, kutoa lugha isiyofaa na kushawishi watu kutenda makosa.

Hata hivyo, wakili anayewatetea washtakiwa hao, Rainery Songea aliliambia gazeti hili jana kuwa ingawa wateja wake walipata dhamana, hadi jana jioni walikuwa mahabusu baada ya barua za wadhamini wao kubainika na makosa.

Wengine waliokamatwa na kufikishwa mahakamani ni naibu mkurugenzi wa habari, mawasiliano kwa umma Bara, Mbarara Maharagande na mwenyekiti Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Abuu Mjaka.

Songea alieleza kuwa wateja wake walikamatwa Novemba 20 mkoani Lindi wakidaiwa kutenda makosa mbalimbali ambayo ni kutishia, kutoa lugha isiyofaa na kushawishi watu kufanya makosa.

“Mheshimiwa Bungara yeye pekee yake alikuwa na makosa mawili; kwanza kufanya mkutano ndani ya mita 200 kwenye vituo vya kupigia kura wakati wa uchaguzi wa marudio wa ubunge wa jimbo la Liwale na kosa jingine ni kutotii amri halali ya polisi,” alieleza.

Wakili huyo alifafanua kuwa kulingana na makosa hayo, mbunge huyo alifanikiwa kutimiza masharti, lakini alikwama kwenye mashtaka yanayomkabili pamoja na wenzake.

Songea aliitaja masharti ya dhamana ambayo washtakiwa walitakiwa kuyatimiza kuwa ni wadhamini wawili wanaoaminika watakaosaini hati ya maandishi yenye thamani ya Sh1 milioni kila moja.

“Masharti walikidhi lakini kilichojitokeza ni makosa madogo katika barua za wadhamini wao. Tuna imani kesho (leo) kila kitu kitakuwa vizuri na washtakiwa hawa watakuwa nje,” alidai Songea.



Chanzo: mwananchi.co.tz