Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bosi wizara ya afya Tanzania, mwenzake wakabiliwa na mashtaka 280

90979 Pic+afya Bosi wizara ya afya Tanzania, mwenzake wakabiliwa na mashtaka 280

Tue, 7 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mhasibu wa Wizara ya Afya nchini Tanzania, Luis Lyimo (54) na Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Christian Social Services Commission, Peter Maduki (61) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka 280.

Mawakili wa Serikali ya Tanzania, Zakaria Ndaskoi na Genes Tesha wamewasomea mashtaka washtakiwa hao leo Jumatatu Januari 6, 2020 huku wakipokezana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 150 ya kughushi, 128 kuwasilisha nyaraka za uongo, moja la wizi  na moja la kutakatisha fedha.

Wakili Ndaskoi amedai washtakiwa hao walitenda makosa hayo kati ya mwaka 2017 na mwaka 2019 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, Tanzania.

Amedai washtakiwa hao kwa nafasi zao wakiwa na nia ovu walighushi hundi mbalimbali zenye thamani ya mamilioni ya fedha na kusaini kwa jina la Upendo Mwingira bila ridhaa yake huku wakijaribu kuonyesha mshtakiwa, Luis Lymo alikuwa akilipwa na taasisi ya Christian Social Services Commission Fedha hizo kama kamisheni wakati si kweli.

Katika mashtaka ya kuwasilisha nyaraka za uongo washtakiwa hao wanadaiwa kuwasilisha nyaraka mbalimbali walizozighushi katika benki ya Standard Chartered.

Pia, washtakiwa hao kwa nyakati tofauti wanadaiwa kuandaa taarifa ya fedha ya uongo wakionyesha akaunti yenye namba 01080002404200 iliyopo katika benki ya Standard Charterd NIC Life House ilikuwa na zaidi ya Sh1.7 bilioni wakati wakijua ni uongo.

 

Katika shtaka la wizi kati ya Machi 30 mwaka 2017 na Oktoba 2018 katika benki hiyo washtakiwa hao waliiba zaidi ya Sh1 bilioni mali ya taasisi ya Christian Social Services Commission.

Kwa upande wa shtaka la utakatishaji fedha, washtakiwa hao wanadaiwa kutakatisha kiasi hicho cha Fedha cha zaidi ya Sh1 bilioni wakati wakijua fedha hizo zilitokana na kosa la kughushi.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hao hawakuruhusiwa kuongeza chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikilizwa kesi ya uhujumu uchumi.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulidai upelelezi bado haujakamilika.

Kwa mujibu wa sheria shtaka la utakatishaji wa fedha pia halina dhamana hivyo washtakiwa walipelekwa rumande na kesi imeahirishwa mpaka Januari20 2020 kwa ajili ya kutajwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz