Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bosi wa Jatu aendelea kusota rumande

Jatu Picsss Bosi wa Jatu aendelea kusota rumande

Mon, 23 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya (33) anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mawili likiwemo la kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu, anaendelea kusota rumande kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokukamilika.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka katika Saccos ya Jatu kwa madai kuwa fedha hizo atazipanda kwenye kilimo cha mazao ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua kuwa ni uongo.

Leo, Oktoba 23, 2023 wakili wa Serikali, Frank Michael ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Wakili Michael ametoa maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

"Mheshimiwa hakimu, kutokana na upelelezi wa kesi hii kutokukamilika, upande wa mashtaka tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amedai Wakili Michael.

Hakimu Mrio baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 6, 2023 itakapotajwa.

Kesi hiyo imeendeshwa kwa njia ya video, huku mshtakiwa akiwa rumande.

Gasaya yupo rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili, halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Itakumbukwa kuwa Aprili 23, 2023, Gasaya alimwandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka ( DPP) akiomba kukiri mashtaka yake na kuomba apunguziwe adhabu.

Julai 31, 2023 mshtakiwa huyo aliondoa nia yake ya kufanya majadiliano na DPP ya kuimaliza kesi yake kwa madai kuwa barua aliyokuwa ameandika ya kuomba kukiri mashtaka na kuiwasilisha upande wa mashtaka, haionekani.

Katika shtaka la kwanza, mshtakiwa anadaiwa, katika ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika Jiji la Dar es Salaam, akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh5,139,865,733 kutoka Saccos ya JATU.

Mshtakiwa wanadaiwa kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu kutoka Saccos ya JATU kwa kujipambanua kwamba fedha hiyo ataipanda kwenye kilimo cha mazao, jambo ambalo alijua kuwa siyo kweli.

Shtaka la pili ni kutakatisha fedha tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika Jiji la Dar es salaam.

Siku hiyo ya tukio na eneo hilo, mshtakiwa akiwa Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa Jatu Saccos, alijihusisha na muamala wa Sh 5,139,865,733 kutoka katika akaunti ya Jatu Saccos iliyopo benki ya NMB tawi la Temeke kwenda katika akaunti ya Jatu PLC liyopo katika Benki ya NMB tawi la Temeke, wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live