Dar Es Salaam. Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathimini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru), Kulthum Mansoor ameanza upya mchakato wa majadiliano na Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania ( DPP) ili kuimaliza kesi hiyo.
Hatua hiyo inatokana na mchakato wa awali kutofikia muafaka.
Mansoor anakabiliwa na mashtaka nane katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu likiwemo la utakatishaji wa Sh1.4bilioni
Mansoor kupitia wakili wake, Elia Mwingira ameleza hayo leo Jumatatu Machi 2, 2020 muda mfupi baada ya kesi inayomkabili mteja wake kuahirishwa.
Akiwa nje ya mahakama, Mwingira aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Kulthum ameshaandika barua nyingine ya kukiri na kuomba msamaha kwa DPP ili kesi hiyo iweze kuisha.
"Mteja wangu ameanza upya mchakato wa majadiliano na tayari ameshamuandikia barua nyingine DPP ya kutaka kumaliza kesi hii,” amesema Mwingira.
Habari zinazohusiana na hii
- Mazungumzo Kulthum Mansoor wa Takukuru, DDP yagonga ukuta
- VIDEO: Aliyekuwa mkurugenzi Takukuru alala mahabusu, kufikishwa mahakamani leo
- Kulthum Mansooor wa Takukuru amwandikia DPP barua ya kukiri makosa
- Aliyekuwa mkurugenzi Takukuru apandishwa mahakamani
Hii ni mara ya pili kwa Kulthum kuandika barua, kwani Oktoba 2019 mshtakiwa huyo aliandika barua ya kukiri mashtaka na kuomba msamaha kwa DPP lakini walishindwa kufikia muafaka.
Januari 6, 2020, wakili Mwingira aliiambia mahakama kuwa waliandika barua ya kukiri na kuomba msamaha kwa DPP lakini walishindwa kufikia makubaliano.
Mwingira amedai kutokana na kushindwa kufikia makubaliano, waliomba upande wa mashtaka kuhakikisha kuwa upelelezi wa kesi hiyo unakamilika kwa wakati.
Leo wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon alieleza Mahakama kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa na hakimu anayesikiliza Godfrey Isaya ana udhuru.
Simon amedai mbele ya Hakimu Mkazi, Vicky Mwaikambo kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea, anaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Mwaikambo ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 16, 2020 itakapotajwa tena.
Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu ya hati ya mashtaka, inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari 2013 na Mei 2018, mshtakiwa alighushi barua ya ofa ya Agosti 13, 2003 kwa madhumuni ya kuonyesha kuwa, barua hiyo imetolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo huku akijua kuwa sio kweli.
Katika shtaka la pili, inadaiwa kati ya Januari 2012 na Mei 2017, Upanga Wilaya ya Ilala mshtakiwa kwa kudanganya alijipatia Sh5.2 milioni kutoka kwa Alex Mavika ambaye ni mfanyakazi wa Takukuru kama malipo ya kiwanja kilichopo kijiji cha Ukuni Bagamoyo.
Katika mashtaka ya utakatishaji fedha, inadaiwa kati ya Januari mwaka 2013 na Mei 2019 maeneo ya Upanga, mshtakiwa alijipatia Sh1,477,243,000 wakati akijua kuwa fedha hizo ni haramu na ni zao la kosa tangulizi la kughushi.