Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bosi Takukuru aanza kazi na mtuhumiwa sakata la viwanja

19946 Takukuru+pic TanzaniaWeb

Mon, 1 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Diwani Athuman amesema anakaribia kukamilisha majukumu aliyopewa na Rais John Magufuli ikiwa ni pamoja na upelelezi wa kigogo wa taasisi hiyo ya kuzuia na kupambana na rushwa anayetuhumiwa kudhulumu viwanja wafanyakazi wenzake.

Diwani, ambaye ni Kamishna wa Jeshi la Polisi, amesema tayari ameshaanza kufanyia kazi maagizo mengine aliyopewa na Rais Magufuli, hasa suala la kuangalia muundo wa Takukuru ili uweke bayana majukumu ya naibu mkurugenzi wa taasisi hiyo.

Tuhuma dhidi ya kigogo huyo anayejulikana kwa jina la Kulthum Mansoor, zilizungumziwa na Rais Magufuli Septemba 12 wakati akimuapisha Diwani kuwa bosi mpya wa Takukuru kuchukua nafasi ya Valentino Mlowola, na siku hiyo alimuagiza kuchukua hatua za kushughulia masuala tofauti, likiwamo la kumfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo na kufanyia kazi suala la majukumu ya naibu wake.

Kulthum ni Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa Takukuru, lakini kwa sasa amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma kadhaa.

Kulthum anadaiwa kuwaahidi wafanyakazi wa taasisi pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wapatao 200, viwanja vilivyopo wilayani Bagamoyo na kuwauzia kwa bei ya kati ya Sh3 milioni na Sh7 milioni, lakini hakuweza kutimiza ahadi yake kutokana na eneo alilotarajia kuuza kuwa na mgogoro na hivyo kulazimika kuanza kuwarejeshea fedha wachache.

Hata hivyo, urejeshaji huo ulikuwa wa mafungu na kusababisha baadhi ya waliochelewa kupata fedha kuanza kutoa malalamiko na hatimaye kufikisha suala hilo kwa uongozi wa Takukuru.

Katika mazungumzo na Mwananchi mwanzoni mwa mwezi uliopita, Kulthum alikiri kudaiwa viwanja na wafanyakazi hao, lakini akaeleza kuwa mchakato wa kuwarejeshea fedha zao alishauanza.

Mapema wiki hii, Kamishna Athuman aliliambia Mwananchi kuwa utekelezaji wa maagizo hayo ya Rais Magufuli unaendelea vizuri.

“Tuko hatua za mwisho za uchunguzi na ukikamilika tu tutampeleka mahakamani. Lengo ni kwenda mahakamani,” alisema Diwani aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kabla ya uteuzi wake kutenguliwa mwishoni mwa mwaka juzi, ikiwa ni takriban mwaka mmoja tangu kuteuliwa kushika nafasi hiyo Jeshi la Polisi.

Katika maagizo yake, Rais Magufuli aliwataka viongozi wa Takukuru kuacha kuoneana aibu, akitoa mfano wa sakata hilo na kusema hadi sasa anayetuhumiwa kuwatapeli viwanja wafanyakazi wenzake, hajafikishwa mahakamani.

“Yuko mama amewadhulumu viwanja watu wa Takukuru, viwanja vyenye thamani ya Sh1.5 bilioni na ni mkurugenzi, lakini wala hajapelekwa mahakamani. Kwa hiyo muache kuoneana aibu, suala la rushwa lazima tulishughulikie,” alisema Rais.

Kuhusu mabadiliko ya muundo wa Takukuru, Diwani pia alisema suala hilo liko katika hatua za mwisho.

Rais Magufuli aliitaka taasisi hiyo kuangalia upya majukumu ya viongozi wake, akitoa mfano wa naibu mkurugenzi, ambaye hutegemea kupangiwa kazi na Mkurugenzi Mkuu Takukuru.

Sheria iliyoanzisha chombo hicho inawataja vigogo hao wawili, lakini imejikita zaidi kuzungumzia majukumu ya mkurugenzi mkuu ambaye huweza kukaimisha kazi zake kwa watu wengine kama wa chini yake au maofisa wa Jeshi la Polisi.

Rais pia alimtaka kushughulikia watendaji wa taasisi hiyo wasiofanya kazi kwa tija na wanaojihusisha na rushwa.

“Tuko ngazi ya mwisho na tushapeleka (suala hilo) utumishi kwa hatua nyingine,” alisema Diwani.

“Lakini maagizo ambayo Rais Magufuli alinipa, matano au sita tushaanza kuyafanyia kazi kwa sehemu kubwa.”

Ingawa hakuwa tayari kuyabainisha mabadiliko hayo, lakini Mwananchi limedokezwa kuwa Doreen Kapwani aliyekuwa miongoni mwa watumishi wanne wa taasisi hiyo waliosimamishwa kazi Desemba 16, 2015, amerejeshwa katika wadhifa wake wa Ofisa Habari wa Takukuru.

Watumishi wengine ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu na Rukia Nikitas ambao kwa pamoja Rais Magufuli aliagiza wasimamishwe kazi baada ya kusafiri nje ya nchi bila ya kibali cha safari kutoka kwa Ikulu. Hata hivyo wote hawa walirejeshwa baada ya kipindi kifupi.

Nafasi ya Doreen ilichukuliwa na Mussa Misalamba ambaye katika mazungumzo na Mwananchi alisema amepangiwa majukumu mengine kwa kuwa kwa sasa Doreen ndio “msemaji wetu (Takukuru)”.

Diwani hakutaka kuzungumzia utekelezaji wa majukumu hayo.

“Bado uchunguzi unafanyika, sitaweza kueleza zaidi. (Uchunguzi) Utakapokamilika, utajua,” alisema Diwani.

Chanzo: mwananchi.co.tz