Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bosi Rubada jela miaka 14

D9786d8dca2fea5d9c361acd5d1cdf44 Bosi Rubada jela miaka 14

Thu, 17 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemuhukumu aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Bonde la Rufiji (Rubada), Aloyce Masanja, kutumikia kifungo cha miaka 14 jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa Sh milioni 86.

Mahakama hiyo pia imemtaka Masanja alipe fidia ya Sh milioni 86 kwa kampuni mbili za kilimo zilizoingiza fedha kwa mshitakiwa huyo.

Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando alisema upande wa mashitaka ulipeleka mahakamani mashahidi watano na upande wa utetezi ulikuwa na mashahidi wawili.

Alisema upande wa mashitaka umethibitisha mashitaka hayo bila kuacha shaka yoyote kwa kuwa kupitia ushahidi uliotolewa mahakamani, umebainisha kuwa kampuni mbili zilitakiwa kuingiza fedha katika akaunti ya Rubada lakini mshitakiwa alighushi na fedha hizo ziliingia kwenye akaunti yake ya kampuni ya Farm (T) Ltd.

"Mshitakiwa alikuwa mtumishi wa umma na katika ushahidi umebainisha kuwa alighushi nyaraka na kutaka fedha hizo ziingizwe kwenye akaunti yake binafsi badala ya kuingia kwenye akaunti ya Rubada. Mshitakiwa ndiye aliingia makubaliano na kampuni hizo na moja ya masharti ni fedha kuingizwa kwenye akaunti ya Rubada," alisema Hakimu Mmbando.

Alisema Sh milioni 86 ziliingia kwenye akaunti ya Farm (T) Ltd licha ya kwamba Rubada ilitamka kwamba fedha hizo zimeingia kwenye akaunti zake jambo ambalo walikuwa wanajua si kweli.

Alisisitiza kuwa endapo fedha hizo zingeingia kwenye akaunti ya Rubada kesi hiyo isingekuwepo.

"Baada ya kupitia ushahidi wote Mahakama imebaini kuwa upande wa mashitaka umethibitisha mashitaka haya bila kuacha shaka kwamba mshitakiwa aliibia fedha za Rubada na mahakama inamtia hatiani kwa mashitaka yote," alisema.

Upande wa utetezi, uliomba mahakama hiyo kupunguza adhabu kwa mshitakiwa kwa sababu ni kosa la kwanza, ana familia inayomtegemea na anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari.

Hakimu Mmbando alisema kwa kila kosa mshitakiwa atatakiwa kutumikia kifungo cha miaka 14 na kwamba adhabu itakwenda kwa pamoja na atatakiwa kulipa fidia ya Sh milioni 86 na endapo wakishindwa, upande wa mashitaka una haki ya kuuza mali za mshitakiwa ili walipwe.

Upande wa utetezi ulidai anakusudia kukata rufaa. Masanja anadaiwa kati ya Agosti mosi hadi 10 mwaka 2010 katika Jiji la Dar es Salaam, mshitakiwa huyo akiwa mtumishi wa umma na wadhifa alionao aliiba Sh milioni 50 zilizofika kwake kulingana na nafasi yake ya ajira.

Katika mashitaka ya pili inadaiwa Masanja kati ya Novemba 10 hadi 30 mwaka 2010 aliiba Sh milioni 36 zilizofika kwake kulingana na nafasi yake ya ajira.

Chanzo: habarileo.co.tz