Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bodaboda adaiwa kuua mwanaye, atenganisha kichwa na kiwiliwili

Kifo Kifo Mauiaji.png Bodaboda adaiwa kuua mwanaye, atenganisha kichwa na kiwiliwili

Wed, 24 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia dereva wa bodaboda Amedius Mfoi (25), mkazi wa Muriet kwa tuhuma za kumuua kwa kumchinja mtoto wake, Amani mwenye umri wa miaka mitatu kwa kumtenganisha kichwa na kiwiliwili.

Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo ya leo Januari 24, 2024 imesema mtuhumiwa alifanya mauaji hayo Januari 23, 2024 saa 12 jioni katika mtaa wa Muriet, jijini Arusha.

Kamanda Masejo amesema mtuhumiwa baada ya kumkata shingo mtoto kwa kitu chenye ncha kali alitenganisha kichwa na kiwiliwili na kisha kuviweka kwenye ndoo za maji na kufunika.

"Baada ya kupata taarifa jana jioni, polisi ilifika eneo la tukio na kuchukua vipande vya mwili huo na kuanza uchunguzi kumtafuta mtuhumiwa ambaye alikamatwa mtaani," amesema.

Amesema bado wanafanya uchunguzi wa tukio hilo kubaini sababu ya kutekeleza mauaji hayo kwa ajili ya hatua za kisheria.

Isack Mfoi, babu wa marehemu amesema Januari 23, 2024 asubuhi waliamka familia nzima wakiwa salama na kila mmoja akatawanyika kwenda kwenye majukumu yake.

Amesema baada ya kurejea alishangazwa kutokumuona mjukuu wake na alipomuuliza mwanaye, hakupata jibu.

"Hapa nyumbani naishi mimi na mke wangu, huyu mtoto wetu Amedeus, mwanaye huwa anapenda kuja hapa kwangu kuangalia runinga, lakini nishangaa jioni hiyo hakuja. Nilipomuuliza (mtuhumiwa) mjukuu wangu leo yuko wapi, alinijibu hajui alipo," amesema Mfoi na kuongeza:

"Basi jioni hiyo tulitoka kuanza kumtafuta kwa majirani bila mafanikio, lakini yeye alikuwa amekaa tu, ndipo nilipomfukuza naye akamtafute, maana tulimwacha naye nyumbani."

Amesema baada ya mtuhumiwa kutoka, alisikia harufu ya kuungua maharage yaliyokuwa yamebandikwa jikoni na katika harakati za kutafuta maji, ndipo alipokuta kichwa cha mjukuu wake kwenye moja ya ndoo za maji.

"Hakika niliogopa sana, nikaita majirani kushuhudia tukio hilo," amesema.

Amesema waliingia kwenye chumba cha kijana huyo na kukuta damu mbichi zimetapakaa kitandani, ndipo walienda Kituo cha Polisi Muriet kutoa taarifa.

Polisi walipofika walikuta kiwiliwili kikiwa ndani ya ndoo nyingine ambazo walizichukua na kuondoka nazo.

"Baada ya kuondoka na mwili, walianza kumsaka mtuhumiwa, ambaye alipatikana na waliondoka naye," amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live