Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bodaboda 38,276 zavunja sheria ndani ya mwezi

Bodaboda Pulled Over 660x400.jpeg Bodaboda 38,276 zavunja sheria ndani ya mwezi

Sun, 15 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Wilbroad Mutafungwa amesema jumla ya waendesha pikipiki kwa ajili ya abiria wapatao 38,276 wamekamatwa ndani ya kipindi cha mwezi mmoja (Aprili hadi Mei) kwa makosa ya kuvunja sheria za barabarani.

Kamanda Mutafungwa ameeleza hayo jana alipokuwa mjini Geita kuendelea na oparesheni ya kitaifa ya ukaguzi wa uvunjwaji wa sheria za barabarani na kulitaja kundi hilo kuwa miongoni mwa vyanzo vikubwa vya ajali za barabarani.

Alisema waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda wanachangia sana ajali kutokana na kutoheshimu sheria za usalama barabarani ikiwemo kupakia abiria zaidi ya mmoja (mshikaki), mwendo mkali na kutoheshimu vivuko vya watembea kwa miguu.

Kamanda Mutafungwa alieleza kuwa katika oparesheni hiyo pia wamekamata pikipiki 6,520 zikiwa hazina bima huku madereva 9,931 wa pikipiki na maguta wakikutwa na makosa ya kutovaa kofia ngumu za usalama. “Eneo hili kusema ukweli ni eneo linalohitaji nguvu kubwa, kwa sababu waendesha pikipiki wengi wanapoteza maisha kwa sababu tu ya elimu ya kuvaa kofia ngumu. Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani tunaendelea kuwapa elimu,” alisema.

Alibainisha kuwa, jumla ya magari 128,014 yamekaguliwa kati ya hayo magari 48,889 yamekutwa na makosa ya ubovu, magari 6,769 yamekutwa na makosa ya bima na magari 9,107 yamekutwa na makosa ya kuzidisha abiria.

Alisema pia madereva 17,916 wamekamatwa kwa makosa ya mwendokasi, madereva 494 wamekutwa na makosa ya ulevi, huku jumla ya abiria na madereva 6,591 wakikutwa na makosa ya kutokufunga mkanda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live