Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Binti kidato cha 1 atiwa mimba, Polisi lawamani

7d16edf3d4df43fcf453907eb9451d47 Binti kidato cha 1 atiwa mimba, Polisi lawamani

Mon, 20 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

Wananchi wa kijiji cha Ugala, Kata ya Ugala, wilayani Urambo wameilalamikia Polisi kwa kutomchukulia hatua mwananchi anayedaiwa kumpa ujauzito mwanafunzi wa kidato cha kwanza mwenye umri wa miaka 16.

Mtuhumiwa katika shauri hilo ametajwa kwa jina la Omary Kishoka (25), mkazi wa kata hiyo. Mwenyekiti wa kijiji hicho, Saidi Shabani Mgalula alisema kuwa baada ya kupokea tuhuma hizo ofisini kwake alimtuma mgambo wa kijiji kumkamata mtuhumiwa, wakamhoji na baadaye akapelekwa kituo cha polisi.

“Tulipopata taarifa za binti huyo kupewa mimba tulifuatilia na baadaye kumtuma mgambo ambaye alifika na kumkamata na tulipomuhoji mwanzo alikataa lakini baadae akakubali na ndipo tulipochukua hatua za kumfikisha kituo cha polisi ili sheria ifuate mkondo wake,”alisema.

Mjumbe wa kamati inayopambana na ukatili kwa wanawake na watoto iitwayo Mtakuwa, Hamidu Usantu alisema alisema kwa kushirikiana serikali ya kijiji wanaendele kufuatilia suala hilo.

Alisema: “Sisi kama kamati ya Mtakuwa, tupo bega kwa bega na serikali ya kijiji tunafuatilia suala hili mpaka pale mwisho na tumekuwa tukifanya kazi kwa ushirikiano kwa maana hata suala hili lilipotokea mtakuwa tulishirikishwa”.

Baba mzazi wa binti huyo, Yasini Rashidi alisema baada ya kesi hiyo kufikishwa kituo cha polisi, walishauriwa wafikie mwafaka wakapinga.

“Kweli alipelekwa kituoni lakini na sisi wazazi tuliitwa na kuulizwa maswali tukatoa maelezo yetu lakini mwisho wake tuliambiwa tukae pamoja ili tulimalize suala hili, sisi tukawaambia kwamba hatupo tayari kuelewana na kusamehe bali tunaiachia sheria ichuke mkondo wake kwani binti yetu yupo tu nyumbani na ndoto zake zimeishia hapa,” alisema Rashidi.

Inadaiwa kuwa hadi sasa malalamiko hayo yapo kwenye Jeshi la Polisi Wilaya ya Urambo kitengo cha upelelezi na mtuhumiwa huyo kijijini Ugala na wakashangaa hakuna kinachoendelea.

Chanzo: habarileo.co.tz