Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Binti asimulia polisi alivyomvua nguo mbele ya baba yake Serengeti

Polisi Pic Data (2) Binti asimulia polisi alivyomvua nguo mbele ya baba yake Serengeti

Sun, 25 Sep 2022 Chanzo: Mwananchi

Tabitha Mwise (22), binti wa Mwise Simon (54), mmoja wa watu watatu waliouwawa kwa kupigwa risasi na polisi wilayani Serengeti kwa tuhuma za ujambazi amesimulia tukio la polisi kuvamia nyumbani kwao kumtia mbaroni baba yake ambaye sasa ni marehemu.

“Kwanza walifika kwa kishindo alfajiri ya Septemba 21, mwaka huu wakiwa na magari mawili; wakavunja milango na kuwatoa nje wote waliokuwemo ndani huku wakimtembezea kipigo kila aliyekuwa mbele yao,” amesema binti huyo

Amesema mlango wake ulipovunjwa na yeye kutolewa nje kwa vipigo, alimkuta baba yake na ndugu wengine wakiwa tayari wametolewa nje huku wakipigwa kulazimishwa kuonyesa silaha zilipofichwa.

“Baada ya kuwajibu kwamba sifahamu bunduki ilipo na wala sijawahi kumwona baba yangu akiwa na bunduki, askari wale waliendelea kunishambulia sehemu mbalimbali za mwili huku watuamuru mimi na baba kuvua nguo zote,” amesema Tabitha akionyesha huzuni usoni kabla ya kushindwa kuendelea kusimulia tukio hilo

Binti huyo ametoa simulizi hiyo mjini Musoma leo Septemba 25, 2022 wakati familia mbili kati ya tatu zilizopoteza wapendwa wao katika tukio hilo walipokutana na waandishi wa habari kusisitiza msimamo wa kutozika hadi uchunguzi huru na wa kina ufanyike kujua sababu na jinsi ndugu zao walivyopigwa risasi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Longinus Tibishiwanu hakupatikana kuzungumzia tuhuma za askari wake kudaiwa kuwavua nguo baba na binti yake mbele ya wanafamilia wengine baada ya msaidizi wake aliyepokea simu yake ya kiganjani kueleza kuwa kiongozi huyo alikuwa kwenye ibada.

Related Ndugu waliouawa na polisi wataka uchunguzi wa kina Polisi yakiri kuua watu watatu SerengetiAdvertisement Msimamo wa familia

Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma, familia ya Mwise Simon na Mgare Mokiri wamesisitiza kutozika hadi uchunguzi wa kina utakapofanyika kubaini sababu na mazingira ya vifo vya ndugu zao.

"Tume huru tunayoomba iundwe ichunguze siyo tu mauaji ya Serengeti, bali pia ya watu wengine waliofia katika mikono ya polisi katika matukio mbalimbali wakiwemo wale waliodaiwa kuwa ni Panya Road," alisema Catherine Ruge, ambaye ni mpwa wa marehemu Mwise Simon

Catherine ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bavicha) amemwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati suala hilo kama alivyofanya kwa kifo cha mfanyabiashara wa madini Mussa Hamisi wa Mtwara aliyefia mikononi mwa polisi.

Watu hao waliouwawa na askari polisi kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Simiyu na Tarime/Rorya ambao walikuwa wanafanya operesheni ya kusaka watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi.

Mwingine aliyepigwa risasi katika tukio hilo lililotokea usiku wa kumakia Septemba 22, mwaka huu ni Mairo Togoro (56) ambaye familia yake haikuwepo kwenye mkutano wa waandishi wa habari mjini Musoma.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Longinus Tibishiwanu alisema watu hao walipigwa risasi walipojaribu kutoroka walipoenda na askari polisi kuonyesha maficha yao na eneo wanakohifadhi silaha walizodaiwa kuzitumia kwenye uhalifu.

Taarifa hiyo inadai watu hao ambao sasa ni marehemu walikuwa wanatuhumiwa kujihusisha na matukio ya ujambazi na waliwaongoza askari kwenda kuonyesha walipojificha wenzao watatu lakini walipofika kitongoji cha Gentamome, ghafla askari polisi walishambuliwa ndipo walipolazimika kujibu mapigo.

Chanzo: Mwananchi