Zikiwa zimepita siku kadhaa tangu kutokea kwa tukio la mauaji ya mama mmoja tajiri wa madini huko mkoani Arusha ambapo aliyemuua ni kijana wake wa kiume aliakua anagombea apewe gari la thamani, huko mkoani Kilimanjaro binti Wendy Patrick anashikiliwa na Polisi kwa kumuua mama yake takribani Mwaka mmoja uliopita akitaka achukue mafao ya mama yake baada ya kustaafu.
Taarifa za jeshi la polisi zinasema kuwa Wendy pamoja na washtakiwa wengine ambao ni waganga wa kienyeji walikua wakimtibu mama huyo na kumtaka atoe pesa nyingi kwa kila aina ya matibabu, mpaka mama huyo alipogundua kuwa mwanae anashirikiana na waganga hao kumuibia, ndipo binti yake aliamua kumtoa uhai ili amiliki pesa zote.
Mabaki ya mwili unaotajwa kuwa wa muuguzi mstaafu Patricia Ibrock, mkazi wa Mjini Moshi mkoani Kilimanjaro yamekutwa yakiwa yamezungushiwa blanket baada ya kufukuliwa kwenye shimo alipofukiwa baada ya kudaiwa kuuawa na mtoto wake kike aitwaye Wendrick Mrema.
Taarifa za Jeshi la polisi zinasema silaha aina ya Panga imekutwa katika shimo ikiwa na mabaki ya mwili unaotajwa kuwa wa Patricia Ibrock huku kukiwa na nywele katika sehemu ya ncha.
Panga hili linadaiwa kuhusika katika kutoa uhai wa mama huyo kabla ya kufukiwa katika shimo la futi mbili kando ya mti wa mwembe nyumbani kwa mama huyu anayedaiwa kuuawa.
Itataarifiwa kuwa ni takribani miezi 10 ndugu na majirani walipokuwa wamuulizia mama huyo na kupatiwa majibu na binti huyo kuwa amesafiri kwa matibabu nje ya nchi.
Jeshi la Polisi limeufukua Mwili huo Januari 9, 2022 katika kata ya Rau baada ya kumhoji binti huyo kwa zaidi ya wiki mbili sasa na hatimaye kukiri kumchinja mama yake kwa panga na kumfukia nyumbani hapo.
Akizingumza na waandishi wa habari, Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Ndg Juma Raibu ameonesha kusikitishwa na kitendo hicho na amelaani vikali tabia ya vijana kuendekeza tamaa na kukosa uvumilivu wa utafutaji Mali na kuishia kufanya matendo ya kinyama.
“Kiukweli hili ni tukio la kutisha, nitoe pole Kwa familia ndugu na majirani wote mliofika hapa, nimepata huzuni sana kuona jinsi gani ya taamaa Mali imetufikisha hapa, nalaani na ninatoa wito Kwa vijana wenzangu wote nchini kuacha kupaparikia Mali na starehe mwisho wake tunageuka kuwa wanyama kiasi hiki, yaani unamuua mama mzazi? Aliuliza.
“Hivi unakuwa hauogopi laana na adhabu ya mola? nalipongeza Jeshi letu la Polisi Kwa hatua hii nawatia Moyo mwendelee na kazi hii njema ya kufichua na kudhibiti wahalifu wa namna hii na wanaoshirikiana nao.” Alimalizia Meya Raibu.
Tukio hilo bado lipo mikononi mwa polisi na madaktari wanaendelea kufanyia uchunguzi Mwili huo kwajili ya hatua zinazofuata.