Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Binamu wa marehemu Aneth alivyomtetea mjane wa Bilionea Msuya

Msuya Msdf Binamu wa marehemu Aneth alivyomtetea mjane wa Bilionea Msuya

Fri, 3 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Binamu wa marehemu Aneth Elisaria Msuya, ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuwa mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji ya Aneth; Miriam Steven Mrita, hakuwahi kutoka Arusha mwezi Mei, 2016.

Pia binamu huyo wa marehemu Aneth; Karim Issa Mruma (45), ameieleza Mahakama hiyo kuwa gari inayodaiwa kuwa alikwenda nayo kwa marehemu Aneth iko gereji ambako ilipelekwa siku sita kabla ya tarehe inayodaiwa kuonekana nyumbani kwa marehemu Aneth, na kwamba mpaka sasa haijawahi kutoka huko.

Mruma, ambaye ni mkazi wa Arusha alieleza hayo leo wakati akitoa ushahidi katika kesi ya mauaji ya binamu yake huyo, akiwa ni shahidi wa pili wa upande wa utetezi.

Aneth aliuawa Mei 26, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam.

Alikuwa mdogo wa aliyekuwa mfanyabiashara wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, Wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, Agosti 7, 2013.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya jinai namba 103 ya mwaka 2018, inayosikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki ni Miriam, ambaye ni mjane wa Bilionea Msuya na mwezake Revocatus Everist Muyella, maarufu kama Ray.

Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, Miriam na mwenzake walikwenda Kigamboni kwa marehemu Aneth mara ya kwanza Mei 15, 206, wakiwa na gari aina ya Ford Rangers (T307 CBH) kwa ajili ya kufanya mipango ya mauaji hayo.

Ushahidi huo ulitolewa kwa nyakati tofauti na shahidi wa 22, Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Arusha, Mrakibu Mwandaimizi wa Polisi (SSP), David Mhanaya kutokana na maelezo ya aliyekuwa mfanyakazi wa ndani wa marehwmu Aneth, Getruda Peniel Mfuru.

Getruda ambaye ni shahidi wa 25 na wa mwisho wa upande wa mashtaka pia alirudia maelezo hayo katika ushahidi wake, akidai kuwa washtakiwa walikwenda huko na akaonana nao mara tatu kwa siku tofauti na wakiwa na magari tofauti.

Hata hivyo katika ushahidi wake akiongozwa na wakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala, shahidi huyo wa pili wa upande wa utetezi, Mruma alieleza mahakama kuwa yeye alikuwa dereva wa Miriam na ndiye aliyekuwa akimuendesha katika safari zake za ndani na za nje.

Mruma ambaye alieleza kuwa marehemu Bilionea Msuya na marehemu Aneth walikuwa ni binamu zake, watoto wa mjomba wake, alidai kuwa kwa mwezi wote wa Mei mshtakiwa wa kwanza, Miriam hakusafiri bali alikuwa Arusha.

"Mwezi Mei wote 2016 Miriam hakusafiri, alikuwa Arusha. Naongea hivyo maana hakuna mtu mwingine aliyekuwa anasafiri naye na akiwa Arusha lazima aje kazini, na hata kama hayupo lazima watu wajue kuwa hayupo maana hawatamuona kazini," alidai Mruma.

Kuhusu gari hilo ambalo aina ya Ford Rangers T307 CBH, ambalo linadaiwa kuwa ndilo washtakiwa alikwenda nalo Kigamboni kwa simu ya kwanza wakati wanapatafuta nyumbani kwa Aneth, Mei 15, 2016, shahidi huyo alidai kuwa gari hilo lilo gereji tangu Mei 9, 2016.

Katika ushahidi wake huo Mruma alidai kuwa alianza kumuendesha Miriam tangu mwaka 2010.

Alifafanua kuwa awali alikuwa dereva wa baba mkwe wake (Miriam) Simoni Elia Msuya, yaani mjomba wake na baadaye marehemu Bilionea Msuya akamchukua na kwamba hivyo alikuwa anawaendesha wote.

Akizungumzia gari T307CBH aina ya Ford Ranger, alidai kuwa anaifahamu maana yeye ndio alikuwa naipeleka gereji na magari mengine yote ya kampuni.

Alidai kuwa gari hilo tangu liliponunuliwa kutoka kampuni ya CMC Motors Arusha, lilikuwa na matatizo ya kimakemia kwenye injini na kwamba lilikuwa linasumbua kila mara, na yeye ndio alikuwa anaipeleka CMC Motors kwa marekebisho.

Alidai kuwa Februari mwishoni mwaka 2016, alilipeleka gari hilo CMC kwa ajili ya ‘service’ maana kesho yake lilikuwa linakwenda Nairobi na Miriam, kuwapeleka watoto shuleni na kwamba siku ya safari alikwenda Nairobi na gari hilo likiendeshwa na Holii kwa kuwa yeye hakuwa mwenyeji njia hiyo.

Mruma alidai kuwa Miriam na Holii walirejea baada ya siku tatu lakini gari likawa limeapata tatizo kwa kuwa injini ilikuwa inagonga na lilikaa nyumbani kwa muda kabla ya kulipeleka CMC Motor.

"Lilikaa kama wiki hivi, nikaichukua tukawa tunazunguka nayo pale mjini kama wiki tatu hivi, ikasumbua tena kwani ilileta shida tena kwenye injini. Nikaipeleka CMC Mei 9, 2016 ndio mpaka leo haijatoka." alidai shahidi Mruma.

Baada ya maelezo hayo shahidi huyo alihojiwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Paul Kimweri maswali ya dodoso na maswali ya ufafanuzi kutoka kwa Wakili Nehemiah Nkoko anayemuwakilishwa mshtakiwa wa pili, Muyella. Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo;

Maswali ya dodoso

Wakili Kimweri: Umesema ulipeleka hii gari gereji baada ya kutoka Arusha, kutoka hapo SG Hotel uliipelekaje?

Shahidi: Nilikuwa naiendesha lakini ilikuwa inagonga kwenye injini.

Wakili: Sasa huyu bosi wako unayemuita Miriam ameshatoa ushahidi hapa kuwa hii gari ilivutwa na watu wa CMC, unakubaliana naye?

Shahidi: Mimi ndio niliipeleka

Wakili: Kwa hiyo siyo kweli maelezo yaliyotolewa hapa na Miriam?

Shahidi: Sijui, maana mimi ndio niliipeleka.

Wakili: Kwa hiyo unaiambia mahakama kuwa hii gari haikupelekwa kwa kuvutwa?

Shahidi: Ndio

Wakili: Hapa mahakamani Miriam alisema ilipelekwa CMC mwezi wa pili, wewe ni sahihi?

Shahidi: Niliipeleka mwezi wa pili na nilikwambia kwamba ilikuwa inakwenda inarudi.

Wakili: Ushahidi wa Miriamu ni kwamba ilipelekwa mwezi wa pili na mpaka leo haijatoka sasa wewe iambie mahakama kuwa maelezo kuwa ilipelekwa CMC tangu Februari na haijatoka mpaka leo siyo ya kweli au maelezo yapi si ya kweli?

Shahidi: Ya Februari si ya kweli.

Wakili: Hawa mabosi wako wote wanajua kuendesha?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Kwa kuwa unakiri ni madereva wanajua kuendesha, utakubaliana nami kuwa si mara zote huwa unawaendesha, kuna nyakati huwa wanaendesha wenyewe?

Shahidi: Sahihi

Wakili: Na wanapokuwa wanaendesha wenyewe huwa hujui wanakwenda wapi?

Shahidi: Sahihi.

Wakili: Siku ambayo Erasto Msuya aliuawa ulikuwa unamuendesha wewe?

Shahidi: Hapana

Wakili: Na unajua aliendesha gari gani?

Shahidi: Sijui

Wakili: Hao mabosi uliokuwa unawatumikia walikuwa na magari mangapi ya familia?

Shahidi: Nakumbuka Rangerover Vogue, Rangerover Autobiograp na Suzuki Tanapa, hayo matatu ndio yanatumika.

Wakili: Haya ndio yalikuwa yanatumika na mabosi wako yote?

Shahidi: Kila mtu kuna gari alikuwa anapenda.

Wakili: Umeieleza mahakama kuna nyakati ambazo huwa wanaendesha wenyewe na kwamba wanakokwenda huwa hupafahamu, ikiwa bosi wako Miriam anatumia gari lingine, huwa unajua?

Shahidi: Ndio

Wakili: Kila anaposafiri anakwambia?

Shahidi: Anaposafiri nje ya Arusha lazima mimi ndio huwa nasafiri naye.

Wakili: Nairobi ni nje au si nje ya Arusha?

Shahidi: Ni nje

Wakili: Akiwa Nairobi akitoka na kwenda sehemu nyingine huwa unajua?

Shahidi: Huwa sijui.

Wakili: Miriam katika ushahidi wake wote hajasema mwezi wa tano wote hajatoka alikuwepo Arusha tu hilo unakubaliana nalo?

Shahidi: Sasa kama yeye alikwambia alisafiri basi chukua la kwake.

Wakili: Wewe unafahamu chochote kuhusiana na tuhuma za bosi wako?

Shahidi: Ameitwa hapa anatuhumiwa kuwa ameua

Wakili: Amemuua nani?

Shahidi: Wifi yake Aneth.

Wakili: Aneth alishawahi kuishi na kina Miriam?

Shahidi: Muda mrefu sana.

Wakili: Kuanzia mwaka gani?

Shahidi: Mwaka sikumbuki lakini ilikuwa kabla mimi sijaanza kufanya kazi hapo.

Wakili Nehemia Nkoko: Shahidi, kama nimekusikia vizuri marehemu Aneth alikuwa anakuita nani?

Shahidi: Binamu, mtoto wa mjomba wangu.

Wakili: Nitakuwa sahihi kuwa kifo hiki cha Aneth kiliwauma sana kama wanafamilia?

Shahidi: Ni kweli kabisa.

Wakili: Nitakuwa sahihi kwamba ninyi kama wanafamilia na ukoo wa Msuya hakumja kutoa ushahidi kwa kuwa mnaamini kwamba shemeji yenu huyu (Miriam) na mshtakiwa wa pili hawakuhusika?

Shahidi: Kama hakuna aliyelalamika inamaana hakutenda kosa.

Wakili: Umeulizwa maswali mengi kuhusu gari aina ya Ford Rangers kuwa imehusika katika mauaji hayo, gari hiyo wewe umeoneshwa hapa mahakamani?

Shahidi: Hapana

Wakili: Unaamimi kwamba kwa mwezi wote wa tano (Mei) shemeji yako hajasafiri kuja Dar?

Shahidi: Kwa mimi naamini hivyo.

Baada ya mahojiano hayo Wakili Kibatala aliieza Mahakama kuwa hakuwa na swali la kumuuliza shahidi ili kurekebisha chochote kutokana na maswali ya dodoso, alimaanisha kuwa kwenye madodoso hapakuwa na swali la kuutikisa ushahidi wake.

Kwa upande wake shahidi wa tatu upande wa utetezi, Kelvin Erasto Msuya (26), ameieleza Mahakama kuwa yeye na dada yake Glory kuwa wasimamizi wa mirathi, Oktoba 27, 2021 baada ya mama yao kuondolewa katika jukumu hilo.

Alieleza kuwa walifuatilia katika halmashauri za Arusha, Moshi na Dar es Salaam kujua kama kuna ardhi ambayo baba yao alikuwa anazimiliki au alizowahi kumiliki lakini zikabadilishwa umiliki.

Hata hivyo alieleza kuwa Dar es Salaam na Moshi hawakupata mali yoyote isipokuwa Arusha ndiko baba yao alikuwa anamiliki viwanja na nyumba kadhaa.

Pia alidai baba yao alikuwa na hisa katika kampuni mbili ambazo wanahisa wake ni baba yao, Erasto Elisaria Msuya na mama yao, Miriam Erasto Msuya (jina la ndoa) ambaye jina lake asili Miriam Steven Msuya.

Alieza kuwa taarifa za Mamlaka ya Mapato (TRA) zilionesha kuwa alikuwa anamiliki gari moja tu na kwamba kwenye akaunti za benki zilikuwa zimefungwa.

Kelvin alieleza kuwa baada ya kukamilisha kukusanya mali walizirodhesha wakawasilisha mahakamani fomu hiyo kisha wakafanya mgawo kwa wanufaika, wao watoto, mama yao na kwa upendo waliwagawia wazazi wa baba yao.

Kelvin alidai kuwa walipeleka mrejesho mahakamani na Jaji Kamuzora aliwauliza wanufaika pamoja na bibi yao kama kuna mtu alikuwa na dukuduku lakini wote walisema kuwa wameridhika na mirathi hiyo ikafungwa rasmi Agosti 11/2022.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live