DAKTARI Deogratius Kalama (36), amedai mahakamani kuwa alimtibu mke wa marehemu Erasto Msuya, Miriam Mrita, baada ya kumweleza ana maumivu ya bega la kushoto na nyonga kwa madai kuwa alipigwa na askari polisi.
Dk. Kalama alitoa ushahidi wake jana katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi ya mauaji ya Anethi Msuya inayomkabili Mrita na mwenzake Revocatus Muyella.
Ushahidi huo unasikilizwa katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam iliyoketi chini ya Jaji Edwin Kakolaki.
Shahidi alidai kuwa Januari 18,2017 alipokuwa ofisini kwake hospitali ya wilaya ya Temeke, walifika askari na wagonjwa wawili mwanamke na mwanamme.
"Nilimsikiliza mgonjwa mwanamke ambaye ni yule pale (alimwonyesha kwa kidole mshtakiwa Mrita), alinieleza anasumbuliwa na maumivu bega la kushoto na nyonga kwa kuwa alipigwa na polisi miezi kadhaa iliyopita," alidai na kuongeza:
"Nilimwandikia vipimo ikiwamo Ex-ray ili nijiridhishe kama ana majeraha kwa ndani, lakini majibu yalionyesha ni maumivu tu ya kawaida, ambayo yanaweza kumpata hata mtu aliyefanya mazoezi" alidai Dk. Kalama.
Akihojiwa na Wakili wa utetezi, Omary Msemo, kama alimsikiliza mgonjwa huyo huku askari wakiwa chumba cha daktari, shahidi alidai wakati anatoa huduma askari walikuwa nje ya mlango wa chumba chake.
Jaji Kakolaki alisema kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa siku tatu na kwamba itaendelea tena Machi, 2022 Msajili atakapopanga tarehe ya kuendelea kusikiliza utetezi wa kesi hiyo ndogo ndani ya kesi ya msingi.
Alisema washtakiwa warudishwe mahabusu mpaka mwakani.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wote wanakabiliwa na shtaka la kumuua kwa makusudi Aneth Msuya, dada wa marehemu bilionea Erasto Msuya Mei 25, 2016 eneo la Kibada Kigamboni, jijini Dar es Salaam.