Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bibi wa miaka 71 auawa na mwanaye kisa kugoma kuuza shamba

Bibi Auawa Ke Bibi wa miaka 71 auawa na mwanaye kisa kugoma kuuza shamba

Fri, 29 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Polisi katika kaunti ya Kisii wanawashikilia washukiwa 10 wakituhumiwa kumteka nyara na kumuua bibi mwenye umri wa miaka 71 aitwaye Yunis Bitengo.

Miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na mtoto wa marehemu aitwaye Moses Abuya ambaye anadaiwa kuwalipa wauaji wa mama yake huyo ambaye ni mjane, baada ya bibi huyo kugoma kukata sehemu ya shamba la familia ili kuliuza.

Wengine wanaozuilia ni mwanamke mmoja anayesemekana kuwa mzee wa kijiji, vijana wengine watatu na wazee watano. Washukiwa hao walikamatwa baada ya barua ya kukiri makosa iliyoandikwa kwa mkono na kijana huyo akiorodhesha majina ya watuhumiwa wenzake aliosaidizana.

Kulingana na barua hiyo iliyopatikana kando ya barabara, mtoto wa marehemu anasemekana kulipa Ksh 4,000 (takribani Tsh 80,000) kwa wauaji wa mama yake ambapo alitakiwa kuongeza kiasi cha Ksh 2,000 (takribani Tsh 40,000) za ziada baada ya kukamilika kwa mpango huo.

Wanakijiji walipata mkono na skafu ya marehemu wakati wa upekuzi huku mwili wake ukiwa haujapatikana wiki nne baada ya tukio hilo.

Kiungo cha mwili wake kilipatikana ndani ya shamba la mahindi, kilomita moja kutoka nyumbani kwake katika kijiji cha Getonto huko Nyakeyo. Juzi Jumanne, wapelelezi walisema bado wanaendelea kuwasaka washukiwa wengine kadhaa.

"Bado tunafuata vielelezo muhimu ambavyo vinaweza kusaidia kukamatwa kwa washukiwa waliosalia; ni suala la muda tu," mmoja wa maofisa wanaoendesha uchunguzi wa tukio hilo alisema.

Bitengo alikuwa akinywa pombe katika nyumba moja kijijini hapo kabla ya kutekwa na wahalifu hao usiku na kuuawa.

Polisi walisema washukiwa ambao tayari wamekamatwa bado hawajafichua sehemu zingine za mwili zilipo.

"Hakuna jiwe litakaloachwa, kila mshukiwa anayehusishwa na mauaji yake na kutoweka kwa mwili baadae wote watafikishwa mahakamani," afisa huyo ambaye hakutaka kufichua utambulisho wake kwa kuhofia kuathiri uchunguzi. Washukiwa hao watafikishwa mahakamani wiki hii.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live