Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bibi amchoma kwa pasi mjukuu kwa dai la kuchana shuka

Ebe6b82f5bc6c0a5ff573119114c8a11 Bibi amchoma kwa pasi mjukuu kwa dai la kuchana shuka

Sun, 6 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MTOTO mwenye umri wa miaka tisa katika halmashauri ya mji wa Bunda, mkoani Mara, amejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kuchomwa na pasi ya umeme na bibi yake kwa madai ya kuchana shuka.

Mwenyekiti wa mtaa wa Saranga, Philpo Safari pamoja na Ofisa Mtendaji wa kata ya Kabarimu, William Magabo, walithibitisha kuwapo tukio hilo nyumbani kwa mtuhumiwa, Juliana Matutu maarufu kwa jina Mama Njara.

Safari alisema kwamba mwanamke huyo anatuhumiwa kufanya ukatili huo Jumapili iliyopita kwa mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya msingi Chiringe B, aliondoka na kwenda kusikojulikana.

“Kwa mujibu ya majirani zake, mwanamke huyo alisema kwamba anakwenda kusalimia msibani, lakini hadi sasa hajulikana alipo” alisema Safari.

Aliyataja maeneo ambayo mtoto huyo aliuunguzwa na pasi hiyo kuwa ni kichwani, miguuni, mikononi na sehemu ya tumboni.

Mwanafunzi aligundulika baada ya kwenda shuleni ambako mwalimu aliyekuwa anasimamia mtihani wa darasa la pili alimuona akiwa anataabika na ndipo akamfuata na kumuuliza kinachomsibu ndipo alieleza undani wa tukio.

Ofisa mtendaji wa kata ya Kabarimu, William Magabo, alifafanua kuwa walimu walimchukua mwanafunzi huyo na kumpeleka katika ofisi ya mtaa serikali za mtaa.

Taarifa ilitolewa polisi sambamba na kumpeleka katika kituo cha afya cha mjini Bunda ambako alitibiwa na kuruhusiwa. Magabo alisema kwa sasa anaishi naye nyumbani kwake kwa usalama wake zaidi, baada ya kukabidhiwa na walimu wake.

Aidha, Safari alisema Mkurugenzi wa kituo kimoja cha kulea na kutunza watoto wa aina hiyo cha Nyumba Salama, kilichoko katika wilaya ya Butiama mkoani Mara, Robhi Samwel, ameshakubali kumchukua mtoto huyo alelewe kituoni hapo.

Babu wa mtoto huyo, alisema kuwa wamekuwa wakiishi nyumbani hapo na mjukuu wao bila matatizo . Alishutumu kitendo alichofanya mtuhumiwa ambaye ni mdogo wake, akisema ni cha kikatili na aibu.

“Tumekuwa tukiishi vizuri hapa nyumbani na huyu mjukuu wetu bila tatizo lolote sasa siku hiyo nilishangaa sana ndugu yangu kufanya kitendo hicho cha aibu, sijui alikuwa na presha gani hiyo” alisema mzee huyo mwenye umri wa miaka 76.

Mtoto huyo alimwambia mwandishi wa gazeti hili kwamba, chanzo cha kufanyiwa ukatili huo ni shuka aliyokuwa amejifunika usiku huo kuchanika kwa bahati mbaya.

Baadhi ya majirani, akiwamo mkuu wa shina, Jonathan Bwire, wamelaani kitendo hicho, wakisema kuwa ni cha kinyama kinatakiwa kukemewa kwa nguvu zote na watu wote.

Licha ya serikali pamoja na wadau mbalimbali yakiwemo mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kama Kivulini la mkoani Mwanza na Nyumba Salama ya Butiama mkoani Mara kukemea vitendo vya ukatili wa watoto na wanawake, lakini vimeendelea kufanyika.

Chanzo: habarileo.co.tz