Tanga. Serikali imezirasimisha bandari bubu nne kati ya 48 zilizopo mwambao wa Bahari ya Hindi Mkoa wa Tanga ili kuokoa mapato yaliyokuwa yakipotea.
Akizungumza mara baada ya kutembelea bandari ya Tanga, bandari hizo bubu leo Ijumaa Novemba 23, 2018, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye amesema mpaka kufikia Januari 2019, huduma za taasisi za serikali ziwe zimewekwa katika bandari hizo nne.
Amesema lengo la Serikali ni kuziba mianya ya wakwepa kodi, ikiwalenga wanaopitisha bidhaa za magendo katika bandari bubu.
Amesema Tanzania kuna bandari bubu zaidi ya 300, hivyo Serikali ina mkakati wa kufanya msako maalum wa kuhakikisha bandari zote bubu zinakufa ili mapato ya Serikali yaongezeke pamoja na mapato ya mtu mmoja mmoja.
"Ifikapo mwishoni mwa Januari nataka kuona mnaweka ofisi za Serikali katika maeneo yaliyorasimishwa ili tuweze kukusanya kodi ya Serikali,” amesema Nditiye.
Naibu Waziri huyo pia ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi na wafanyabiashara wanaoendelea kutumia bandari bubu hizo waache mara moja kwani hazitambuliki.
Kwa upande wake, meneja wa bandari Mkoani Tanga, Parcival Salama amesema kwa mkoa wa Tanga ni bandari mbili tu ambazo zinatambulika kisheria ambazo ni bandari ya Tanga na bandari ya Pangani.
Salama amezitaja bandari bubu ambazo zimerasimishwa rasmi ni Kipumbwi, Kigombe, Mkwaja zilizopo Pangani na Moa wilayani Mkinga.
Meneja huyo amesema mkoa wa Tanga kuna bandari bubu 48 nakwamba kwa upande wa Mkinga ziko 12 , Tanga Jiji 20, Muheza moja pamoja na wilaya ya Pangani ziko 15.
Mapendekezo ya kurasimisha bandari hizo bubu yametokana na utafiti uliofanywa na menejimenti ya bandari ya Tanga kutokana na maelekezo yaliyotolewa na serikali.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Moa, Rambazo Mohamedi amesema wamefurahishwa na uamuzi wa serikali wa kuamua kuzirasimisha bandari hizo na wako tayari kutoa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za serikali.