Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baba wa kambo atupwa jela miaka 60 kwa kumpa mimba mtoto wa kufikia

Hukumu Pc Data Baba wa kambo atupwa jela miaka 60 kwa kumpa mimba mtoto wa kufikia

Thu, 9 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani iliyoketi jana Lugoba mkoani humo imemhukumu kwenda jela miaka 60 Mrisho Hodari kwa makosa mawili ambayo ni kumbaka na kumpa mimba mwanafunzi wa shule ya msingi.

Mwanafunzi huyo aliyekuwa akisoma darasa la sita Shule ya Msingi Sofu, Halmashauri ya Chalinze imeelezwa kuwa, Mrisho ambaye kwa sasa ameanza kutumikia kifungo hicho alikuwa ni baba yake wa kufikia ambao walikuwa wanaishi kwenye nyumba moja hivyo akatumia mwanya huo kutekeleza kitendo hicho.

Kwa mujibu wa taarifa za hukumu hiyo kutoka mahakama hiyo zimesema kuwa, baada ya mwanafunzi huyo kupata ujauzito na baadaye kumtaja mhusika huyo na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria uliwekwa muda ili kusubiri hadi mtoto alipozaliwa ili kupata vipimo vya vina saba.

“Mtoto alipozaliwa, baada ya vipimo ilibainika kuwa Mrisho ndiye mhusika wa mimba hiyo,”amesema hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo, Sameera Suleiman.

Amesema kuwa ushihidi mwingine mbali na vipimo vya vinasaba ni kupitia kwa mwanafunzi huyo ambavyo vyote kwa pamoja havikuacha shaka yoyote hivyo vikatosheleza matakwa ya kisheria na kumhukumu kutumikia adhabu hiyo.

Hata hivyo, alipotakiwa kujitetea mshtakiwa huyo Mrisho Hodari alikanusha kuhusika na kosa hilo jambo ambalo halikumnasua kukwepa kifungo hicho cha miaka 60 jela.

Akizungumza nje ya mahakama, mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Wivina Alikadi amesema kuwa awali walikuwa wanaishi na mshtakiwa huyo kama mume na mke ambaye alimkuta akiwa na watoto wake wawili wa kike wote aliozaa na mumewe wa kwanza.

“Nimeishi naye miaka kumi na nimezaa naye watoto watatu alinikuta nina watoto wangu wawili wa kike. Tukawa tunaishi pamoja lakini nilishangaa kitendo alichokifanya kumbaka mwanangu na kumpa ujauzito,”amesema.

Amesema kuwa hivi sasa kibarua kinachomkabili ni namna atakavyowahudumia watoto watano na mjukuu mmoja ikilinganisha kuwa hana kipato cha uhakika hivyo kwake ni mtihani.

‘Sijutii kufungwa kwa huyu Mrisho acha aende kwakuwa amenitendea kitendo cha kikatili sana lakini kwa sasa kinachonifikirisha ni jinsi gani nitakavyowahudumia familia ya watoto watano na mjukuu mmoja,” amesema.

Amesema kuwa katika kipindi cha miaka kumi cha maisha yao waliyoishi maeneo mawili tofauti kati ya Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam, walikuwa wanaachiana majukumu kama mmoja akisafiri mwingine anabaki na watoto hivyo huenda hali hiyo ilimfanya mwanaume huyo kuwa na nafasi ya kufanya kitendo hicho.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live